The House of Favourite Newspapers

Uzuri wa Gari Bovu Lipate Mteremko

YAANI shoga yangu leo nimekaa zaidi ya nusu saa natafakari meseji moja tu! Shoga hata kama wanawake tumeumbiwa mateso si kwa aina hii kwa kweli, loooo!

Ngachoka! Kama wasemavyo Wachaga! Shoga hili la leo siyo kunifika hapa tu bali limenifika huku! Kuna wanaume wana roho za kikatili sijawahi kuona. Yupo radhi afurahie na mchepuko lakini kwako uambulie maumivu!

Leo acha niwape vidonge vyenu mkinuna litakuwa limewaingia lakini yangu ya moyoni nimeyatapika, au naongopa shoga? Hatukatai sisi wanawake wakati mwingine akili zetu tunakuwa kama vile tumebebewa na kushindwa kutambua nje ya boksi!

Nasema yote hayo kwa sababu shoga! Nimeamua kuanza kwa kusema gari bovu ili uelewe linakuwaje zuri likipata mteremko! Kuna msomaji amenitumia meseji ya malalamiko ya familia yake, itakuwa vizuri kama nikiianika meseji yake ili nawe upate cha kujifunza;

“Anti kwanza nakupongeza kwa kutuelimisha, kwa muda mrefu nimekuwa nikikufuatilia mada zako! Shoga mimi ni mama wa watoto wawili japokuwa naishi na watoto watatu. Mtoto wangu wa tatu shoga ametoka kwa mama mwingine.

“Kilichonifanya nije hapa shoga ni tabia ambayo kama mwanamke nafanyiwa kila siku, mume wangu alipokuwa akitaka kunioa hakuniweka wazi kama ana mtoto wa nje, nikamkubalia taratibu zikafanyika na kuolewa. Baada ya kupita miaka sita nikiwa nimezalishwa watoto wawili, kuna mwanamke alikuja kumbwaga mtoto wa miaka minne na kusema amezaa na mume wangu.

“Niliumia sana kwa kweli baada ya kumbana mume wangu akakiri, nilijishusha na kuanza kumlea mtoto huyo sawa na wanangu wa kuwazaa, nilimpenda sana.

“Ili kufupisha maelezo shoga, sasa hivi mume wangu amekuwa hashauriki, amerudisha uhusiano na yule mwanamke aliyezaa naye, kila nikimwambia anakuwa mkali na wakati mwingine ananipiga sana. Amenipiga marufuku kumsemea hata kwa wazazi wangu wala wake. “Shoga naomba nisaidie ushauri, naogopa asije akapata mtoto mwingine kisha aje anibwagie.”

Niwageukie nyie wanawake wenzangu, kuna kipindi sawa unakuwa na huruma lakini unaangalia na maisha yako! Mwanaume kama huyo anakuziba mdomo usifike kwa wazazi wako wala wake kisha yeye anaendelea kukufanyia hivyo unasubiri miujiza gani kama siyo kuwa punda wa jangwani?

Hii imekuwa tabia kwa wanaume wengi siyo kwako tu, wakipata mke wa kumuoa huyohuyo wanamrundikia watoto wa nje na mbaya zaidi wanashindwa kuwalea vizuri kwa kutegemea mke aliyenaye ndiyo kila kitu. Yaani wamekuwa wakiwachukulia wake zao kama gari bovu vile, wanaliegeshea kwenye mteremko liserereke lenyewe!

Shoga nimeumia! Nimeumia! Nimeumia! Nimetamani sana nikutane na huyo mwanaume nimpe mfano wa wanawake tulivyo kama Anti Nasra hajaita Anti Ng’aa! Na sisi wanawake jamani, mwanamke unatakiwa kuwa na maamuzi yako inapofikia hatua kama hii! Sawa mwanaume ana haki ya kukutawala lakini siyo kwa kupitiliza kiasi hiki, shuuuutuuuuuu!

Ukiona unamuelimisha na haelimishiki basi chukua hatua. Usitake akushike masikio, akupake na mate kabisa mwisho wa siku akakugeuza zege, kutwa kunyamaza kwake anafurahi kwako unaugulia maumivu, looo! Kwa leo naomba niishie hapa maana si kwa kuniharibia siku yangu. Ni mimi Anti Nasra Shangingi Mstaafu.

Comments are closed.