Kartra

Vanessa Aacha Alama 5 Bongo Fleva

KAMA unafuatilia muziki wa Tanzania, bila shaka utakuwa unafahamu alichokifanya Vanessa Mdee au V Money kwenye muziki huo.

 

Vanessa mwenye sauti ya maridhawa alianzia kwenye utangazaji, lakini ilipofika mwaka 2013, aliamua kugeuza shilingi na kuingia kwenye muziki baada ya kuachia wimbo wake wa Closer ambao ulimtambulisha vyema.

 

Tangu aanze muziki miaka nane iliyopita, Vanessa alifanya kazi na wasanii wakubwa Afrika kama Reekado Banks, Mr P, KO, Distruction Boyz na wengineo na kolabo hizo zimesababisha atambilike mno kuzoa tuzo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania kama AFRIMMA na nyinginezo.

 

Kwa sasa anaishi na mchumba’ke, Rotimi kule Atlanta nchini Marekani akitarajia kupata mtoto wa kiume, lakini siyo mbaya kujikumbushia nyimbo zake tano za Bongo Fleva ambazo zimeacha alama kwenye muziki huo.

 

1; JUU-VANESSA FT JUX

Juu ni wimbo wa mapenzi ambao Vanessa aliuachia Desemba, 2016 na Watanzania waliupokea kwa mikono miwili. Hilo lilithibitishwa kipindi Vanessa na Jux walipokuwa kwenye tamasha lao la pamoja la In Love and Money Tour mwaka 2018 kwani wimbo huo ulikuwa unapagawisha mashabiki mara tu ulipokuwa unatumbuizwa na wanamuziki hao jukwaani.

Hadi sasa,video ya wimbo huo imeshatazamwa mara zaidi ya milioni 4.4 kwenye Mtandao wa YouTube.

 

2; NEVER EVER-VANESSA

Ilipofika mwaka 2015, Vanessa aliungana na prodyuza Nahreel kufanya Wimbo wa Never Ever. Wimbo huo ulithibitisha kuwa yeye ndiye malkia wa muziki wa RnB nchini Tanzania kutokana na namna ambavyo aliimba vizuri na kwa hisia mno. Kusindikiza Never Ever, Vanessa aliachia video ya wimbo huo iliyofanyika nchini Johannesburg nchini Afrika Kusini na kufikia sasa umeshatazamwa mara zaidi ya milioni 3.5 kwenye Mtandao wa YouTube.

 

3; WET-VANESSA FT G NAKO

Wimbo wa Wet ni mahususi kabisa kwa watu wanaopenda muziki wa kuchangamka. Kipindi wimbo huu ulipotoka, ulichezwa mno kwenye kabu za starehe ndani na nje ya Tanzania. Ubunifu wa Rapa G Nako aliyetawala kwenye kiitikio pamoja na mdundo wenye nguvu kutoka kwa Nahreel, vilitosha kabisa kuufanya Wet usichuje kwenye masikio ya msikilizaji. Wimbo huo umeshatazamwa mara zaidi ya milioni 4.4 kwenye Mtandao wa YouTube.

 

4; KISELA-VANESSA FT MR P

Kisela ni wimbo ambao Vanessa anaimba kwa hisia kali mno. Katika moja ya mahojiano yake, Vanessa alikiri kuwa alikuwa analia wakati anarekodi wimbo huo kutokana na kubeba maana kubwa mno kwake. Ekelly kutoka Nigeria ndiye amehusika kuandaa wimbo huo huku Director Clarence akihusika kwenye video ambayo hadi kufikia sasa imeshatazamwa mara zaidi ya milioni 3 kwenye YouTube.

 

5; THATS FOR ME-VANESSA FT DISTRUCTION BOYS & PRINCE BULO

Ndani ya Thats For Me, Vanessa anajiachia na kuonesha ufundi wake kwenye kudansi huku akisindikizwa na mdundo wa nguvu kutoka Afrika Kusini. Hadi sasa wimbo huo umetazamwa mara zaidi ya sabini na nane elfu kwenye YouTube.

STORI; ELVAN STAMBULI


Toa comment