VANESSA MDEE NA JUX ACHENI KUTUZUGA!

VANESSA MDEE NA JUX kiki

 

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunizawadia pumzi yake ambayo imeniwezesha kuandika barua hii ya leo inayokufikia wewe msomaji ambaye pia umekuwa ukinisaidia kwa maoni na ushauri kuhusu safu yetu hii.

 

Leo nina kazi ya kuzungumza na wanamuziki wawili ambao kwa muda mrefu, wametengeneza moja kati ya kapo bomba kabisa za wasanii wanaojihusisha kimapenzi. Unapozungumza kuhusu wasanii wanaofanya vizuri kwa sasa katika Bongo Fleva, huwezi kuwaacha kando Jux na Vanessa ambaye ni maarufu kama Vee Money, kwani hivi sasa ni miongoni mwa vijana wanaotupa uwakilishi mzuri kimataifa, kwa sababu kazi zake ni moto barani Afrika. Binafsi ninawakubali, maana mimi pia ni muumini mkubwa wa aina ya muziki wanaofanya.

 

Maisha ya kimapenzi ya wasanii hawa siku za nyuma, leo yamenisukuma niseme nao kidogo, hasa kwa kuangalia matukio yanayoendelea hivi sasa kati yao. Uhusiano wao uliingia dosari kwa namna ambayo hakuna hata shabiki mmoja alitegemea, maana ni kama kitu cha ghafla na ambacho hakikutolewa maelezo kiasi cha kuwatosheleza wafuasi wao.

 

Siku hizi ni vigumu kidogo kuamini moja kwa moja mambo yanayotokea, hasa yanayohusisha mapenzi, maana vijana wa siku hizi wanajijua wenyewe na akili zao. Wanaweza kutengeneza kitu cha kushangaza, ukaingia mkenge halafu kesho yake unawaona watu wameshikana viuno maisha yanaendelea.

 

Kama unadhani ni mambo ya mzaha, waone Idriss Sultan na Wema Sepetu walivyofanya, hivi ukiambiwa wanaendelea na mapenzi utakataa vipi? Usikute mchana wanawahadaa watu lakini usiku mnene ukifika wanakuwa wote kama zamani.

 

Kukicha wanaonekana mahasimu, kukikuchwa wapenzi, mambo ya kutafuta kiki! Ninasema hivi kwa sababu ukifuatilia sana mambo yanayoendelea baina ya wawili hawa, unapata picha kama vile kuna kitu nyuma ya pazia.

 

Unawasilikiza katika mahojiano yao na vyombo mbalimbali vya habari kuhusu uhusiano wao, unashindwa kuelewa sababu hasa iliyowakosanisha. Hakuna mtu anayekwenda moja kwa moja, ni kama wanakwepakwepa hivi kusema kitu ambacho kinawaweka mashabiki wao njia panda.

 

Vanessa kwenye mahojiano yako, ambayo nimekuwa nikiya-tazama au kusikia, hakuna sababu ya msingi ambayo umewahi kuizungumza juu ya Jux, mtu akikuangalia kile unachokizungumza na sura yako ni kama maigizo fulani hivi.

 

Sikiliza wimbo wa Vanessa, Kisela na zile mbili za Jux, Umenikamata na Utaniua, ni kama vile wanatumiana ujumbe baina yao, kitu kinacho-onyesha bado kuna mahaba ya dhati kwa mwenzake. Ni kama wapenzi wawili ambao baada ya mzozo mdogo kati yao, sasa kila mmoja anaogopa kujishusha na kumuomba msamaha mwenzake. Wanasahau kuwa mapenzi hayana ustaa, hayana pesa, hayana elimu wala hayana vyeo.

 

Ninachotaka kuwaambia hawa vijana wenzangu ni kuwa kama kuna mmoja anajihisi ndiye chanzo, basi ajishushe na kumuomba mwenzake msamaha ili nafsi zetu zifurahi, siyo kama hivi mnavyowayumbisha mashabiki ambao hawajui kama mnacheza
mchezo gani.

 

Kupendana mnapenda ila sijui nini kinawazuia, au ndiyo aina ya kiki mliyoamua kuja nayo tofauti na zile kiki za kishamba za wavaa nusu utupu? Kama bado mnapendana
mna nafasi ya kurudiana kwa sababu hakuna mwanadamu aliyekamilika hasa katika eneo la mapenzi. Jux, mdogo wangu mrudie shemeji yetu, kwa sababu maneno huumba, nahofia Wimbo wa Utaniua usije ukawa kweli bhana!

 

Lakini nawe shemeji Vanessa ni heri ukamuambia ukweli Jux, maisha yake ya kisela ambayo hutaki au hupendi aendelee kuyafanya. Kwa nini uteseke wakati unaweza kumrudia mtu ambaye unajua anakupa furaha na amani ya moyo wako?

 

Acheni kuwazuga mashabiki wa muziki wenu, kama kuna tatizo kati yenu ni muda wa kukaa na kusawazisha kwa sababu ninyi si wa kwanza kukorofisha, kugombana na kisha kutengana.

 

Cha kufanya kila mtu ajichunguze ni wapi alikosea, maana ninachokiona ni kama mapenzi mnayachukulia kistaa, kitu ambacho ni ngumu mno kufanikiwa.

 

Nyinyi ni moja ya kapo za wapenzi iliyobamba kwa wasanii, kila mtu alipenda mlivyopendeza, samehehaneni, maana nyimbo zenu hizi zinaonyesha hisia zenu, malizeni tofauti muwape mashabiki

 

MAKALA: GABRIEL NG’OSHA| RISASI


Loading...

Toa comment