The House of Favourite Newspapers

Vanessa nusu utupu inakuwaje ‘brand’ kwako?

0

vanessa

Vanessa Mdee, ‘Vee Money’

NIKIRI wazi, simjui ki-hivyo Vanessa Mdee, ‘Vee Money’, ila kama mdau wa muziki, naheshimu kazi zake chache alizofanya, ambazo zimemuweka katika daraja lenye hadhi katika Bongo Fleva.
Licha ya umri wake mdogo (amezaliwa Juni 7, 1988) anaonekana amefanya mambo mengi makubwa, yakiwemo kufanya kazi katika vyombo kadhaa vya habari alipohusika kuwahoji watu wengi maarufu duniani, kutoa neno katika mikutano mikubwa ya kimataifa ya vijana iliyofanyika katika mataifa mbalimbali Afrika, Ulaya na Marekani.

Historia yake inamuonesha, licha ya kuzaliwa Arusha, ule mji wetu wenye vivutio vingi vya kitalii, pia amekulia katika nchi nyingi tofauti Afrika na nje ya bara hili, ambako bila shaka amejifunza mila, utamaduni na desturi za watu wengi tofauti.

Nilimsikia kwa mara ya kwanza katika muziki mwaka 2012 kama sikosei, katika wimbo wa Ommy Dimpoz wa Me and You. Ukisikiliza vizuri kibao kile, unafahamu fika kuwa yule mdada anaijua vizuri hii lugha iliyokuja kwa ndege, Kiingereza.
Kwa mara ya kwanza, nilimuona ‘live’ wiki chache zilizopita, alipotembelea chumba cha habari cha gazeti hili na kufanya mahojiano na kituo chetu cha televisheni mtandaoni, Global tv online. Kwa mazungumzo yake siku hiyo ni binti ambaye yupo vizuri kichwani, kwa maana anajitambua!
Siku chache baadaye, nikaona habari yake katika mtandao mmoja maarufu wa habari za muziki na mastaa wa Bongo, akisema kuwa staili yake ya kuvaa nguo fupi ni katika kulenga kutengeneza brand yake, kwani ana malengo nayo siku zijazo.

Mtazame hata katika video za nyimbo zake nyingi ni mtu mwenye kupenda mavazi ya Kimagharibi, yale ambayo kitovu siyo kiungo chenye tofauti na kiwiko cha mkono!
Well, kila mtu ana malengo yake na inapotokea hivyo kwa vijana kama Vee Money ni jambo la kujivunia kuwa katika umri huo, amelenga kuwa mtu f’lani siku zijazo. Si watu wengi wa umri wake wanafikiri kuwa akina nani siku zijazo zaidi ya kuyumba na upepo, leo wanataka kuwa kama John Magufuli, kesho kama Edward Lowassa keshokutwa kama Reginald Mengi na mtondogoo kama Beyonce!
Lakini kama msanii, kwa maoni yangu, suala la kuwekeza katika nguo fupi, haliendani na mila na desturi za Kitanzania, hasa kwa watoto wa kike. Nakumbuka, hata alipofika chumba cha Habari cha Global Publishers, alikuwa akikaa kwa shida kutokana na ufupi wa nguo aliyovaa.

Kama lengo ni dili za ‘mbele’ kama wenyewe mnavyosema, nadhani ilikuwa ni busara kama angekaa kimya na hilo kubakia moyoni mwake, lakini kuvaa nguo fupi mbele ya wazazi, kaka na dada zako kwa sababu tu unalenga kitu f’lani mbele ya safari, siyo jambo la kujivunia kwa binti wa Kitanzania.

Kitakachomfanya yeye kuwa brand ya watu kuvutika naye, ni kazi yake, wala siyo muonekano wake. Tunawapigia kelele wale wadada wa Bongo Muvi, siyo kwa sababu tunawaonea wivu na muonekano wao mzuri wakiwa katika mavazi ya nusu utupu, bali kwa kuwa hawalisaidii taifa katika kutengeneza maadili yanayotakiwa, ambayo ndiyo kazi yao kubwa kama vioo vya jamii.

Leave A Reply