VIAZI VITAMU VINAPUNGUZA KASI YA KUZEEKA, KISUKARI

VIAZI vitamu au mbatata vikiliwa vinastawisha mwili hasa ngozi bila kujali ni ya mwanamke au mwanaume hasa vile visivyowekewa vinasaba kwa lengo la kuongeza kiwango chake cha vitamin A ya asili. 

 

Viazi vitamu ni miongoni mwa vyakula vya wanga vyenye faida mwilini kwa sababu vina viini lishe na dawa lishe zinazoweza kukinga na kutibu baadhi ya maradhi. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Chakula na Dawa, nchini Marekani (U.S. FDA) imebainisha kiazi kimoja kikubwa kinaweza kumpatia mtu asilimia 100 ya Vitamini A inayohitajika mwilini kila siku akikila.

 

Unapokula viazi vitamu unapata vitamin nyingi tofauti kama vile vitamini A, C, B5, B6, C, E. Lakini pia ukila viazi vitamu unapata madini ya potasiumu, magneziamu, fosforasi, manganese, zinki, wanga, sukari ya asili, nyuzi lishe, beta-carotene na choline zinazosaidia kustawisha ngozi ya mwanadamu na kuifanya nzuri.

Viazi vitamu ukivila pia husaidia mtu kupata usingizi mzuri usio na mauzauza. Taasisi ya Afya ya Marekani (NIH) inasema Vitamini A inayopatikana kwenye viazi vitamu inasaidia kupunguza kasi ya kuzeeka. Taasisi hiyo ya Kimarekani imethibitisha pia kwamba mlaji wa viazi vitamu anaimarisha afya ya macho yake.

 

Hata hivyo, daktari bingwa wa macho kutoka Hospitali ya Duke, Jill Koury anasema upunguvu wa Vitamini A unasababisha sehemu ya jicho inayopokea mwanga kuharibika na kusababisha uoni hafifu.

 

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kitivo cha Sayansi ya Lishe cha Harvard, Shule Kuu ya Afya ya Jamii (HSPH), beta- Carotene inayopatikana kwenye viazi inapunguza uwezekano wa kupata saratani ya utumbo na tezi dume. Pia, dawa lishe aina ya beta-Carotene inayopatikana kwenye viazi husaidia sana kudhibiti maradhi ya moyo, pumu na kupunguza kasi ya mwili kuchakaa.

 

Utafiti huo pia ulibainisha dawa lishe hiyo huwasaidia wanawake kutengeneza vichocheo muhimu wakati wa ujauzito na kunyonyesha. Utafiti umebaini kuwa madini ya potasiamu yaliyopo ndani ya viazi hivyo inasaidia kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu, yaani high blood pressure.

Viazi vitamu vinasaidia kuondoa madini yasiyohitajika mwilini, kuboresha ufanyaji kazi wa moyo, kuboresha mapafu, kuimarisha kinga ya mwili na ni chanzo kikubwa cha beta-carotene. Faida nyingine ni kwamba viazi vitamu ni chanzo cha madini ya chuma, potassium na calcium.

 

Viazi vitamu vina nyuzinyuzi ambazo husaidia kupunguza kasi ya ufyonzwaji wa sukari kwenye damu. Hii husaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu, kuukinga mwili na kuboresha umeng’enyaji wa chakula. Viazi vitamu pia ni moja ya vyakula ambavyo vinapendekezwa kwa mjamzito kutokana na kuwa na sukari asili ambayo husaidia kuweka sawa kiwango cha insulin mwilini na hivyo kupambana na kisukari.

Uwepo wa kirutubisho cha beta – carotene pia huweza kutumika kama antioxidants ambayo husaidia kupunguza madhara ya maumivu ya viungo, hulinda afya ya mapafu hivyo ni vizuri kutumiwa kwa watu wenye pumu pia. Aidha, viazi vitamu vimesheheni nyuzinyuzi ambazo ni muhimu kwa umeng’enyaji wa chakula tumboni na husaidia kukinga dhidi ya saratani ya utumbo na ukosefu wa choo.

 

Vitamin D, kwenye kiazi kitamu ni muhimu kwa afya ya meno, mifupa, moyo na ngozi na vitamini B6 ni muhimu kwa kuulinda mwili dhidi ya matatizo ya shambulio la moyo na kiharusi. Viazi vitamu ni chanzo kizuri cha madini chuma ambayo husaidia uundaji wa seli nyeupe na nyekundu za damu, hivyo kufanya kuwa na uwezo wa kupambana na tatizo la ukosefu wa damu mwilini (anemia).


Loading...

Toa comment