The House of Favourite Newspapers

Vichwa Viwili vya Binadamu Vyakutwa Shambani

POLISI wilayani Ibanda nchini Uganda, wamekuta vichwa viwili vya binadamu (mwanaume na mwanamke) vikiwa vimetupwa shambani maeneo ya Kyegwisa ambapo ni kilomita tatu kutoka Ibanda mjini.

 

Katika uchunguzi wa awali, polisi wamewaeleza waandishi wa habari kuwa mauaji hayo yatakuwa yalifanyika mbali na eneo ambalo vichwa hivyo vimeokotwa. Hata hivyo, polisi na watu waliojitokeza katika kushuhudia tukio hilo hawakuweza kuvitambua vichwa hivyo ni vya nani.

 

Aidha, tukio hili limetokea baada ya siku kadhaa kupita tangu miili miwili ya mwanamme na mwanamke isiyo na vichwa kukutwa katika msitu wa Kikoyo uliopo Buhanda karibu na wilaya ya Kitagwenda ambapo kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Wilaya, Geofrey Muchunguzi,  amesema miili hiyo haikutambuliwa ni ya nani.

 

Zaidi ya hayo, alisema kuwa watafanya vipimo vya DNA vya miili na vichwa hivyo ili kujiridhisha kama vichwa vilivyopatikana Ibanda ni vya miili hiyo au la.

 

Sambamba na hilo, Kamanda wa Polisi wa Ibanda anaeleza kuwa anaeleza kuwa vichwa hivyo vilivyokutwa shambani vimehifadhiwa katika mochwari ya kituo cha afya cha Ruhoko na vitapelekwa wilayani Kitagwenda kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya DNA ili vitambuliwe.

Comments are closed.