DAR ES SALAAM: KIUNGO wa Tottenham Hotspur, Victor Mugubi Wanyama, raia wa Kenya, jana asubuhi aliwasili nchini Tanzania kwa ajili ya mapumziko ya siku kadhaa baada ya kumaliza majukumu ya timu yake ya taifa.
Wanyama aliyetua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar, amesema amekuja Tanzania kwa sababu katika maisha yake hakuwahi kuifaidi nchi hii kwa kuitembelea zaidi ya kuja mara moja na kuondoka.
Muda mfupi baada ya kutua, Wanyama alizungumza kwa kifupi: “Nitakaa hapa kwa muda mrefu.”
Katika kulizungumzia soka la Tanzania, kiungo huyo aliyeifanikisha Spurs kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya England nyuma ya Chelsea, alisema: “Nafuatilia soka la Tanzania, hivyo najua hapa Tanzania kuna wachezaji wengi wazuri, lakini pia nazijua timu nyingi kama Simba, Yanga na Azam.”
Ujio wa Wanyama, unamfanya kuwa mchezaji wa nne kutua Tanzania hivi karibuni ambapo awali alianza kuja kiungo wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya England, David Beckham. Kisha akafuata beki wa Liverpool, Mamadou Sakho kabla ya kiungo wa Spurs, Christian Eriksen. Wachezaji hao wote wametembelea mbuga mbalimbali za wanyama hapa nchini.
Mwandishi Wetu | CHAMPIONI