The House of Favourite Newspapers

Video: Alichozungumza Prof Kabudi Mkutano Wa 74 Umoja Wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi akihutubia Mkutano wa 74 wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amehutubia Mkutano wa 74 wa Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani mbele ya viongozi wa dunia Ijumaa ya Septemba 27, 2019 na katika hotuba yake hiyo ametilia mkazo mambo matatu ambayo Serikali ya Tanzania inayasimamia.

 

Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na Tanzania kujidhatiti katika kupambana na janga la tabia ya nchi ambapo alisema tayari Tanzania imepiga hatua kubwa na kutolea mfano wa kuhifadhi misitu yake na kujenga bwawa kubwa la umeme litakaloifanya gharama za umeme kuwa nafuu kwa Watanzania wote, kudhibiti ukataji miti hovyo inayotumika kama nishati mbadala na wananchi wengi wa kipato cha chini.

 

“Kwa hiyo tunaungana kabisa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha kwamba nchi zetu zinazoendelea zinasaidiwa kupata maendeleo na wakati huohuo kuhifadhi mazingira. Na maana yake wote tuna wajibu wa pamoja wa kulinda mazingira, lakini kila mtu ana wajibu ulio tofauti.

“Wao waliochafua mazingira lakini sasa wana mali za kutosha, wana wajibu wa kutoa fedha, teknolojia ya kupambana na hiyo hali na sisi tuna wajibu wa kushiriki katika miradi hiyo ili kunusuru na kuiokoa dunia isiangamie mapema kuliko inavyotarajiwa.” Alisema Profesa Kabudi.

 

Aidha Prof Kabudi, alitumia nafasi hiyo kuziomba jumuiya za kimataifa kuliangalia kwa kina suala la Zimbabwe dhidi ya vikwazo ambavyo vimesababisha hali ya maisha ya wananchi wengi nchini humo kuwa ngumu zaidi.

 

Waziri Kabudi pia ameieleza Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni wakati sasa wa Afrika kuwa Bara litakalojiletea maendeleo ya viwanda na kuachana na kasumba ya kuuza malighafi kwenye masoko ya Ulaya badala yake waanze kujenga viwanda ili kuimarisha uchumi na kuwapatia ajira vijana.

 

Kuhusu kile ambacho Tanzania inataka kuona kwenye maeneo ya ulinzi wa amani hususan kule Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako imepeleka askari kwenye kikosi maalum, Waziri Kabudi ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye UNGA 74, amesema: “Tanzania ingependa muhula wa majeshi ya ulinzi wa amani ya MONUSCO uongezwe lakini ile brigedi ambayo Tanzania inashiriki ya kuhakikisha inapambana na magaidi na vikundi vyenye silaha ambayo vinaua watu kule DRC vidhibitiwe.”

Comments are closed.