VIDEO: CHADEMA WATOA TAMKO, TUNDU LISSU KUVULIWA UBUNGE

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji.

Siku mbili baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kutangaza kumvua ubunge aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji, leo Juni 30, 2019 amezungumza na wanahabari akiwa makao makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar na kusema Spika amekosea kwani si kweli kuwa Lissu anapenda kukaa hospitalini.

Dk. Vincent Mashinji amesema: “Tumezitafakari sababu alizotaja Spika kusababisha Lissu kuvuliwa ubunge, mojawapo ni utoro, kwamba Lissu amekuwa mtoro wa mikutano na vikao vya bunge bila taarifa kwa Spika kinyume na taratibu.

 

“Lakini Lissu ni mgonjwa, hajaenda kumsalimia mtu na kutoka, na utaratibu wa matibabu ya mgonjwa anaeujua ni daktari wake, mimi ni daktari ‘by proffessional’ nikimwambia mgonjwa uwe unajiinua kidogo ni moja ya matibabu ila wewe kama hujui utaona huyu anatupotezea muda.

 

“Spika Ndugai mwenyewe aliwahi kuliambia Bunge kuwa atakwenda kumsalimia Lissu kokote atapokuwa iwe hospitalini Nairobi au hospitali nyingine yoyote ingawa hajawahi kufanya hivyo, ila leo anasimama hadharani na kuuambia umma wa Watanzania na dunia nzima kuwa Lissu hajui yuko wapi.

 

“Katika kuokoa uhai wa Lissu, Mheshimiwa Ndugai alishiriki moja kwa moja siku alipopigwa risasi kwa kufika hospitalini na alishiriki kutoa maamuzi ya namna gani Lissu atatibiwa.

 

“Sababu ya pili, amesema Lissu anapenda kukaa hospitali, si kwamba Spika hajui yuko wapi, si kweli kama Lissu ameamua tu kukaa hospitali na sidhani kama kuna mtu kati yetu ana hamu tu ya kwenda kukaa hospitali sasa hivi ila huwa tunalazimika kwa sababu ya ugonjwa.”

Loading...

Toa comment