The House of Favourite Newspapers

Lusinde: Lugola Awahoji Kinana, Nape Kuhusu Sauti Mtandaoni – VIDEO

Mbunge wa Jimbo la Mtera (CCM), Livingstone Lusinde.

MBUNGE wa Jimbo la Mtera (CCM), Livingstone Lusinde,  leo Julai 20, 2019,  ameongea na wanahabari  jijini Dar es Salam  akimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, awaite Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye,  na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana,  ili awahoji kufuatia kipande cha sauti zao kilichosambaa mitandaoni kikidaiwa ni sauti zao wakizungumzia masuala ya kisiasa.

Vilevile, Lusinde amesema ndani ya CCM hakuna mgogoro isipokuwa kuna watu  wachache wanaoulumbana na mtu mmoja mmiliki magazeti nchini,  jambo ambalo haliwezi kuitwa mgogoro ndani ya chama hicho.

Hapo alikuwa akizungumzia waraka ulioandikwa na waliokuwa makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Yusufu Makamba kuhusiana na malalamiko yao dhidi ya mmiliki wa magazeti hapa nchini ajulikanaye kama Cyprian Musiba.

Kwa mujibu wa waraka ambao Kinana na Makamba wameuandika kwenda kwenye uongozi wa chama hicho kupitia kwa Pius Msekwa, wawili hao wanasema Musiba amekuwa akiwaandika akiwazushia mambo mbalimbali ya kisiasa na asichukuliwe hatua yoyote na mamlaka zilizopo.

”Nataka niseme kuwa wazee wangu wamepotoka kwa kutoa waraka  huo; walitakiwa wamtafute kijana wa kumjibu Musiba, au wao wenyewe watafute press (mkutano wa habari) wamjibu Musiba siyo kuandika waraka utakaobaki maishani mwao kwamba viongozi wa kisiasa wa ngazi za juu,  Kinana na Makamba,  waliuandika kumlalamikia Musiba, vitu ambavyo naona vimewafedhehesha sana.” alisema Lusinde.

Kuhusu sauti  zinazodaiwa kuwa ni za Kinana na Nape, alisema zina maneno ya fedheha kwa viongozi wa nchi hii, na ndiyo maana akamtaka Lugola awaite Kinana na Nape awahoji kwa kutoa maneno ya kashfa kuhusiana na uongozi wa nchi hii.

Akigusia msimamo wa aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa awamu ya nne, Bernard Membe, alisema atamshughulikia pindi akirejea kutoka ziara ya kikazi nchini China.

“Bernard Membe namweka kiporo, naenda safari China kwa ziara ya kazi za kibunge, nikirudi nitamshughulikia…  Hana chochote… Nitamkuna panapomwasha,” alisema Lusinde.

Mbunge huyo wa Mtera pia alipendekeza taarifa ya Katibu Mkuu wa CCM, Ally Bashiru, kuhusu wizi wa mali za chama hicho, iwekwe wazi kwenye vyombo vya habari ili wananchi wawajue wale walioiba mali hizo.

“Mwenyekiti wetu (wa CCM) ikimpendeza, ile taarifa ya Dk. Bashiru inayohusu wizi wa mali za CCM irushwe kwenye vyombo vya habari, ili wananchi wawajue walioiba mali za CCM,” alisema Lusinde.

Akitetea kauli zake kuhusu kuitwa na kuhojiwa kwa Kinana na Nape, Lusinde alisema:

“Mimi nafurahi Musiba kuwatukana viongozi wastaafu, sababu Kinana alitukana viongozi wake akawaita mizigo, Nape amepata umashuhuri kwa ajili ya matusi, nashangaa wanakasirika nini wakati wameuunda utaratibu huu.”

Akikanusha kwamba ametumwa kuja kutoa kauli hizo, Lusinde amesema amejituma mwenyewe kulisemea jambo hilo.

“Hakuna mbunge anayepangwa, mimi sihitaji kutumwa na mtu, najituma mwenyewe.  Mimi sijaja kumtetea Musiba, kazi aliyoifanya Musiba ilikuwa inafanywa na Nape,  kwa hiyo wasilalamike hiyo kazi walishaianza wao.

“Kinana na mzee Makamba wana nafasi ya kuzungumza na Rais John Magufuli, hawakuitumia nafasi hiyo, wakaamua kuandika waraka. Hilo halina maana yoyote,” alisisitiza Lusinde.

 

Comments are closed.