The House of Favourite Newspapers

VIDEO: Maswali ya PAPO kwa PAPO Bungeni Kwa WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa wilaya na mikoa kuacha kutumia nguvu katika ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo badala yake watoe elimu juu ya namna ya kupata vitambulisho hivyo pamoja na wanaotakiwa kuwa navyo.

 

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Aprili 25 bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya hapo kwa papo kwa waziri mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga.

 

Haonga alitaka kujua nini kauli ya Serikali kuhusu ugawaji wa vitambulisho hivyo, akisema maeneo mengine wanaopewa si watu husika na kushauri ugawaji huo usitishwe ili ifanyike tathmini ya watu sahihi wanaotakiwa kupatiwa.

 

“Wakuu wa wilaya na mikoa watumie muda wao kuelemisha nani anapaswa kuwa na kitambulisho badala ya kutumia nguvu, kulazimisha au kuwapa wajasiriamali wakubwa na kuondoa maana ya vitambulisho hivi.”

 

“Serikali tumeipokea hii (swali la Haonga) na tutaendelea kutoa maelekezo kwa  wakuu wa wilaya na mikoa ili watumie muda zaidi kuelimisha zaidi kuliko kulazimisha ili kuondoa usumbufu kwa wanaouza mahindi, mchicha maana hawa ndio Rais (John Magufuli)  aliwalenga,” amesema.

 

Majaliwa amesema Serikali imeweka utaratibu mzuri kwa wajasiriamali wadogo kuchangia pato la taifa baada ya Rais kubuni njia ya kuwatambulisha kwa kuweka madaraja ya wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa.

“Serikali imewalenga hawa wadogo ambao kipato chao hakizidi Sh4milioni kwa mwaka ili nao wapate nafasi ya kuchangia pato la taifa lakini pia kuwaondolewa usumbufu kwenye maeneo wanayofanyia biashara kwa kutozwa kodi kila siku na kupunguza mapato yao kwa mwaka.”

 

“Vitambulisho vilivyotolewa kwa wakuu wa wilaya natambua kwamba maeneo mengine utekelezaji wake si mzuri,  wapo wengine wanalazimisha watu badala ya kuwaelemisha namna ya kupata vitambulisho hivyo,” amesema.

Majaliwa amesema kuna maeneo vitambulisho hivyo wanapatiwa wafanyabiashara wakubwa ambao kwa mujibu wa taratibu wao wanalipa kodi kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

 

Akiuliza swali hilo Haonga amesema: “Vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo vimekuwa kero kubwa katika maeneo mbalimbali nchini, hasa wale wanaouza mboga, vitumbua. Kibaya zaidi maeneo mengine hata wanaotoka shambani na kuchuma mchicha wanaambiwa ni wajasiriamali na kutakiwa kutoa Sh 20,000.”

 

“Suala hili kwa mtazamo wangu halijatafsiriwa vyema hasa ngazi za chini kwa wanaolitekeleza. Maana wapiga debe hata walimu hutakiwa kulipa fedha kununua vitambulisho. Hivi huu ugawaji hauwezi kusitishwa kwa muda ili kufanyika tathmini na kujua ni nani aliyelengwa?”

Comments are closed.