Video: Mtoto wa Dudu Baya Aeleza Baba Yake Kupotea – “Hatujui Yuko Wapi”

Baada ya kusambaa kwa taarifa ya kupotelea kusikojulikana kwa takriban miezi miwili kwa msanii wa Bongo Fleva, Godfrey Tumaini ‘Dudu baya’ huku kukiwa na hofu ya kuuawa, mwanaye Maria Godfrey ameibuka na mapya.

 

Maria anayeishi Kirumba jijini Mwanza, ameliambia Gazeti la IJUMAA kuwa, mara ya mwisho kuwasiliana na baba yake huyo, ilikuwa ni Julai 27, mwaka huu alipokuwa Kahama kwa ajili ya shoo.

Anasema kuwa, baada ya hapo alikuwa akijaribu kumpigia simu bila mafanikio.

 

Maria anaendelea kusema kuwa, alipoona kuwa juhudi za kumtafuta baba yake zimegonga mwamba, alimtafuta prodyuza wake ambaye yupo nchini Ujerumani, lakini naye alisema mara ya mwisho, aliwasiliana naye mwezi wa nane (Agosti) mwanzoni, mwaka huu.

 

“Nilipoona kimya, niliamua kumtafuta kwa kila rafiki yake, lakini wanasema hawajamuona wala simu yake haipatikani kabisa, na wengine wakasema walikuwa wananitafuta mimi, ili waniulize kama ninaweza kujua alipo,” anasema Maria kwa uchungu.

 

Maria anasema kuwa, walifanya jitihada za kwenda mpaka nyumbani kwa baba yake, maeneo ya Tegeta jijini Dar, lakini nako walielezwa kwamba, hajaonekana muda mrefu, huku nyumba ikiwa imefungwa.“Kiukweli maisha yangu yamekuwa ni magumu mno, baba yangu alikuwa akinisaidia kwa kila kitu; kuanzia kula yangu na mengine yote, kiukweli sasa hivi ni shida juu ya shida,” anasema Maria.

 

Anaendelea kusema kuwa, mama yake mzazi yupo Dubai na kwa upande wake anatafuta kazi, hivyo kuna wakati analala njaa, maana hata ndugu yake, Willy ambaye pia ni mtoto wa Dudu Baya, naye anatafuta kazi pia.

 

“Yaani maisha yangu yamebadilika ghafla, nalala njaa wakati mwingine kwa sababu yeye alikuwa mkombozi wetu, lakini pia hata kaka yangu Willy, naye anatafuta maisha, lakini hafanyi vizuri kwa sababu baba haonekani,” anasema Maria.

 

Maria aliongezea kuwa, wana mpango wa kwenda Shinyanga, maana mara ya mwisho waliona amepiga picha na mkuu wa mkoa huo, hivyo inawezekana labda aliumwa na yuko huko.

 

“Nataka siku hizi mbili niende Shinyanga, maana alipiga picha na Mkuu wa Mkoa huo ili tumuulize kama anawasiliana naye au vipi, maana inawezekana labda anaumwa yuko huko au ametekwa!” Anahoji Maria akiomba msaada wa vyombo vya habari vya Global kutangaza kupotea kwa baba yake, ili kama kuna mtu mwenye taarifa za alipo, basi ajitokeze.

 

Taarifa za kupotea kwa Dudu Baya, zilianza kusikika baada ya mtoto wake huyo, kuweka kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram kuwa, takriban miezi miwili sasa, hajawasiliana na baba yake huyo na hajui alipo.

Stori:IMELDA MTEMA, Ijuma

⚫️ Kwa UPDATES zote, Download GLOBAL APP:

⚫️ ANDROID:http://bit.ly/38Lluc8

⚫️ iOS:https://apple.co/38HjiCx

Toa comment