The House of Favourite Newspapers

Video: Prof Safari Aanika Udhaifu Vyama Vya Upinzani Nchini

0


ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Prof Abdallah Safari, amesema vyama vya upinzani vina ubinafsi na matokeo yake vimeshindwa kukiangusha Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza mapema leo kwenye kipindi cha Front Page kinachorushwa na +255GlobalRadio, Prof Safari alisema, endapo vyama hivyo visingekuwa na ubinafsi, vingeungana kwa pamoja na kuhakikisha wanasimia ajenda moja ya Tume Huru ya Uchaguzi.

“Utitiri wa vyama huu hauna maana. Vyama hivi ni pandikizi…Mwalimu alisema viungane hivi vyama vipambane na CCM, sisi viongozi wa upinzani tumeshindwa.

“Ndani ya miaka 7 tulimng’oa mkoloni sasa miaka 20 tumeshindwa kuwadai CCM tume huru? Tatizo ni ubinafsi,” alisema Prof Safari.

Profesa Safari alisema kwa kuwa yeye amestaafu anataka akumbukwe kwa jambo moja kubwa ambalo ni Tume Huru ya Uchaguzi.

“Mimi nataka wapinzani wote hasa Cuf na Chadema wanikumbuke kwa jambo moja kubwa sana kwamba ajenda yetu kubwa wapinzani ni kudai Tume Huru ya Uchaguzi,” alisema.

Akizidi kuchambua masuala mbalimbali yanayohusu siasa nchini, Prof Safari alilizungumzia suala la wabunge wa Chadema waliovuliwa ubunge wao na chama hicho kikubwa cha upinzani.

“Wale waliovuliwa uachama hawakupewa haki ya kusikilizwa hivyo uamuzi wa chama haukuwa sahihi. Unapotoka ndani ya chama chako maana yake unakuwa si mbunge hivyo Spika kuwalinda pia sio sahihi,” alisema.

Miongoni mwa wabunge hao, ni Willifred Lwakatare, mbunge wa Bukoba Mjini; Anthony Komu, mbunge wa Moshi Mjini, Joseph Selasini, mbunge wa Rombo na David Silinde, mbunge wa Momba, mkoani Songwe.
Katika maamuzi yake ya kuwafukuza wabunge hao, Chadema kilisema, kimechukua hatua hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa wabunge wote hao, wamekuwa wakikisaliti chama hicho.

Alipoulizwa kuhusu vuguvugu linalozungumzwa kwamba kwa kuwa Rais Dk John Pombe Magufuli amefanya mambo makubwa kwenye nchi hivyo apewe muda zaidi wa kuongoza, Prof Safari alisema ni vizuri Katiba ikafuatwa.

“Nakubaliana na Katiba kwamba baada ya miaka mitano aje kiongozi mwingine. Unajuaje pengine anaweza kutokea mtu mzuri zaidi,” alisema Prof Safari huku akiweka bayana kuwa Rais wake bora ni Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

“Hakuna Rais ambaye amefanya mambo makubwa sana kama Mwalimu lakini wamekuja wengine nyumba ziliuzwa, viwanda kubinafsishwa, kwangu mimi Nyerere anabaki kuwa Icon,”alisema.

Stori: Mwandishi Wetu

Leave A Reply