JPM: Kama Makonda Alitumia Fedha za TASAF Azirejeshe – VIDEO

RAIS John Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuzirjesha fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) iwapo alizichukua, kwani yeye si maskini.

Magufuli ameyasema hayo leo, Februari 17, 2020, jijini Dar es Salaam wakati akizindua kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF.

“Kaya 22,034 zilithibitika wanakaya wake siyo maskini na mojawapo ni akina Makonda ambao walizitumia fedha hizo kwenda Dodoma wakati siyo maskini na ninaomba kama hili ni ukweli Makonda azirudishe hizo fedha,” alisema  Magufuli.

Katika hotuba yake Makonda alieleza jinsi rais mstaafu wa awamu ya tatu,  Benjamin Mkapa, alivyompatia fedha za TASAF na kuzitumia kwenda nazo Dodoma kuomba ridhaa ya kuchaguliwa katika nafasi ya Makamu Mwenyeki wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Pia Magufuli amesema kulingana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), umaskini wa chakula umepungua kutoka asilimia 18.7 mwaka 2001 mpaka asilimia 9.5 mwaka 2017/2018.

Alimpongeza Mkapa kwa kuanzisha mfuko huo na rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuuendeleza na kuongeza kwamba katika kipindi cha miaka 20 ya utekelezaji wa mpango huo kumekuwa na mafanikio mengi kwa jamii.

“Kupitia miradi hiyo wananchi wamenufaika kwa kupata barabara za vijijini, madarasa, nyumba za walimu, madawati, zahanati na manufaa mengine,” amesema.


Loading...

Toa comment