The House of Favourite Newspapers

VIDEO: RAIS MAGUFULI ATOA UJUMBE MZITO KWA WANAJUMUIYA YA SADC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli amefungua maonesho ya wiki ya viwanda kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC).

 

Akizungumza katika hafla hiyo ya Wiki ya Viwanda ya SADC jana, Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema kuwa ili kufikia uchumi wa kati viwanda ni kichochea muhimu katika sekta nyingi kwani uwepo wa viwanda utasababisha uhakika wa uzalishaji na uchakataji wa bidhaa na kufanyabiashara kwa nchi wananchama.

 

Rais Magufuli amezitaka nchi wanachama wa SADC kuweka kipaumbele kwenye kuhuisha teknolojia katika viwanda vilivyoko ndani ya jumuiya ya Maendelea kusini mwa afrika (SADC) pamoja na kushughulikia kwa haraka zaidi vikwazo vinavyochelewesha ukuaji wa viwanda.

 

“Viwanda ni Sekta muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yeyote, kuondoa umasikini, kuongeza ajira na Sekta hii imeziletea Maendeleo makubwa nchi zilizoendelea, kwa hiyo mkutano huu ni dhahiri kuwa sasa nchi za SADC zimeanza kuchukua hatua madhubuti za kukuza sekta hii na ikiwa mkakati huu utatekelezwa utasaidia kukuza uchumi wa nchi zetu”, Rais Magufuli.

 

Akielezea suala la teknolojia Rais Magufuli amesema kuwa ukuzaji wa teknolojia na ubunifu kwenye sekta ya viwanda ni silaha muhimu kwa nchi za SADC kuendelea na kutegemeana kwani utazalisha ajira, biashara kubwa, na kuepuka kuuza malighafi kwa wingi nje ya Afrika kama ilivyosasa.

 

Vilevile, mchango wa sekta ya viwanda kwa nchi za SADC bado ni mdogo kwani Sekta hiyo inachangia wastani wa asilimia 10 ya pato la taifa na katika Jumuiya ya SADC sekta hiyo muhimu inachangia asilimia 11 tu. Amesema Rais Magufuli.

 

Aidha Rais Magufuli alizitaka nchi wanachama wa SADC kujikita zaidi katika kukuza ubunifu na teknolojia rahisi kwenye sekta ya viwanda kwa kuwaendeleza vijana na kuimarisha viwanda vidogo vidogo vilivyoko kwenye jumuiya, kwa hiyo wiki ya viwanda ni fursa muhimu kwa nchi zote wananchama.

 

“Wiki ya Viwanda ya SADC ni fursa ya kubadilishana uzoefu miongoni mwa wadau kuhusu utekelezaji wa mikakati ya miaka 49 ya uendelezaji wa viwanda katika jumuiya yetu, bado tunasafari ndefu kuhakikisha sekta ya viwanda inazidi kukua na kuleta mageuzi ya kiuchumi katika nchi zetu”, Amesema Rais Magufuli

 

Rais Magufuli amesisistiza kwa kusema kuwa katika kuimarisha mashirikiano ndani ya Jumuiya ya Maendeleo (SADC) ni lazima kuimarisha sekta ya uwekezaji kwani nchi hizo zina fursa nyingi kwenye uwekezaji ikiwemo viwanda vya madini, kilimo, uvuvi na ufugaji kwa hiyo wananchi kutoka SADC wanatakiwa kuchangamkia fursa kwenye soko la takribani watu milioni 344.

 

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Innocent Bashungwa amesema kuwa uthubutu wa Rais Magufuli kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati wenye viwanda ni mkubwa na matokea yake yanaonekana sasa. Hivyo, maonesho haya ni moja ya njia muhimu ya kuimarisha sekta ya viwanda nchini.

 

“Maonesho haya ya wiki ya viwanda yanawawezesha wanachama wa SADC kuona namna nchi wenyeji inavyotekeleza uwekezaji kwenye sekta ya Viwanda. Aidha, tunaamini wazalishaji, wafanyabiashara, na wananchi kwa ujumla watachangamkia fursa mbalimbali zitazotokana na mkutano huu wa SADC.”, Waziri Bashungwa.

 

Waziri Bashungwa alisema kuwa Tanzania inafanya vizuri kwenye biashara ndani ya SADC kwani takwimu zinaonyesha kuwa mauzo ya Tanzania kwenda SADC mwaka 2018 yalikuwa dola za kimarekani milioni 999 ikilinganishwa na dola za kimarekani milioni 875 mwaka 2017 ikiwa na ongezeko la asilimia 12.16.

 

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Amina Ally amesema kuwa uthubutu wa Rais Magufuli wa kuendeleza ndoto ya Baba wa Taifa, Mwl . Julius Nyerere kwa kujenga bwawa Kubwa la kufua na kuzalisha umeme mto Rufiji ni hatua kubwa kwa maendeleo ya sekta ya viwanda.

 

Balizo Amina alisema kuwa katika utekelezaji wa miradi yote inayofanywa na Serikali suala muhimu ni uwepo wa amani kwa Tanzania na ndiyo maana ikachaguliwa kuwa mwenyeji wa maonesho ya SADC yakifuatiwa na Mkutano mkuu wa viongozi wakuu wa nchi za wanachama wa SADC.

 

“Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha amani na kwa tukio hili itaendelea kudumisha amani na utilivu kwani mpaka sasa maonesho na mkutano mkuu unaofanyika hapa unaonesha kuwa tanzania ni nchi ya amani”, Waziri wa Viwanda Zanzibar, Amesema Balozi Amina Ally.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt.Stagomena Tax, amesema kuwa juhudi za Serikali ya Tanzania kutekeleza mradi mkubwa wa kufua na kuzalisha umeme mto Rufiji ni moja ya njia madhubuti katika kuimarisha na kukuza sekta ya viwanda kwa Jumuiya ya SADC.

 

“Kutekelezwa kwa Mradi wa umeme mto rufiji tunaamini kuwa Tanzania itazalisha umeme wa kutosha, tunaomba ziada iweze kwenda kwenye nchi wanachama wa SADC kwani kumekuwa na changamoto ya kubwa mgawo wa umeme na uendeshwaji wa viwanda unahitaji mambo mengi ikiwemo umeme huwezi kuwa na viwanda bila kuwa na umeme unaozalishwa kwa urahisi, kwa hiyo Tanzania imechukuia maamuzi mazuri kuzalisha umeme mto Rufiji.”, Stagomena Tax, Katibu Mtendaji, SADC.

Aidha Dkt.Stagomena aliwaomba watanzania kutumia fursa zilizopo nchi wanachama SADC kwa kuwa ni soko kubwa ambalo linajumuisha nchi 16, ambazo zinawatu wapatao milioni 344 na pato la taifa la pamoja la dola za Marekani milioni 2.5 hivyo ni muhimu kwa watanzania kuzijua fursa hizo na kuzitumia ipasavyo.

Maonesho ya Wiki ya Viwanda yanayofanyika Tanzania kuanzia tarehe 05 mpaka 9 Agosti 2019 na kufatiwa na Mkutano wa wakuu wa nchi 16 wanachama utakaofanyika Agosti 17 na 18, 2019, katika Ukumbi wa Julius Nyerere Dar-es-salaam.
Mwisho

 

Comments are closed.