Mama Adaiwa Kumchoma Moto Mwanaye Sehemu za Siri

IRINGA: MZAZI kuchukua kijinga cha moto na kumchoma mwanaye sehemu za siri ni hasira, mhemko au kupagawa na ibilisi? Huu ni mjadala unaopatikana katika habari hii ya kusikitisha.

Jeshi la Polisi mkoani Iringa, linamshikilia Jupista Mhinza (30), mkazi wa Kijiji cha Kilolo kwa tuhuma za kumchoma na kijinga cha moto sehemu za siri mtoto wake wa miaka 6, kwa kosa la kuchelewa kurudi nyumbani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire aliwaeleza waandishi wa habari hivi karibuni ofisini kwake kuwa, tukio hilo limetokea Mei 31, mwaka huu.

“Mtoto huyo alikuwa akicheza na watoto wenzake hivyo kuchelewa kurudi nyumbani kitendo kilichomkwaza mama yake mzazi na kuamua kuanza kumshambulia kwa kipigo na kisha kuamua kumchoma na kijinga cha moto sehemu zake za siri na kumjeruhi vibaya,” alisema kamanda Bwire.

Aliongeza kuwa, mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi Kilolo (jina linahifadhiwa) amelazwa katika Kituo cha Afya cha Kasanga akiendelea na matibabu na mwanamke huyo anashikiliwa na jeshi la polisi na kwamba atafikishwa mahakamani kwa tuhuma hiyo ya kujeruhi.

Amani linawaasa wazazi kujiepusha na hasira zilizopitiliza wanapokuwa wakijenga tabia za watoto wao kwani siku zote adhabu yoyote kwa mtoto inalenga kumfundisha siyo kumuumiza au kumjeruhi.

Stori: Francis Godwin, AMANI

Loading...

Toa comment