Video ya Kusisimua ya Trump huku Mbunge wa Buchosa Eric Shigongo Akiwepo – Video

Rais wa Marekani, Donald Trump, amewataka Wamarekani wamrejee Mungu na kuirejesha dini katika taifa hilo, akidai kuwa wengi wameiacha.
Akitangaza hatua hiyo huku Mbunge wa Buchosa Eric Shigongo akiwa miongoni mwa wahudhuriaji, Trump alisema ameunda kikosi maalum kinachoongozwa na Mwanasheria Mkuu, Pam Bondi, ili kuchunguza “kulengwa” kwa Wakristo, ambao anadai wanakumbana na upinzani kutoka kwa taasisi zisizoamini katika dini yoyote.
Akizungumza katika hafla mbili tofauti jijini Washington katika maadhimisho ya kitaifa Alhamisi, Februari 6, 2025, Trump alisema kikosi kazi hicho kitakuwa na jukumu la “kusitisha mara moja aina zote za kulengwa na kubaguliwa kwa Wakristo ndani ya serikali ya shirikisho.” Alitaja taasisi kama Wizara ya Sheria (DOJ), Mamlaka ya Mapato (IRS), na Shirika la Upelelezi (FBI) kuwa miongoni mwa mashirika yanayodaiwa kuhusika na ubaguzi huo.
Mapema siku hiyo, Rais Trump alihudhuria hafla maalum ya maombi katika Jengo la Bunge la Marekani, hafla ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka kwa zaidi ya miaka 70, ikiwaleta pamoja wabunge wa pande zote kwa maombi na mazungumzo ya kiimani.
Aliwaambia wabunge kuwa uhusiano wake na dini ulibadilika baada ya majaribio mawili ya kumuua kushindikana mwaka jana, na akawahimiza Wamarekani “kumrudisha Mungu” katika maisha yao.
Katika hotuba yake, alitafakari juu ya tukio la risasi lililompata karibu na kumuua kwenye mkutano wa kampeni huko Butler, Pennsylvania, mwaka jana, akisema, “Lilinibadilisha kwa njia fulani, nahisi.”
“Nahisi nimeimarika zaidi,” aliendelea.
“Nilikuwa namwamini Mungu, lakini sasa nahisi imani yangu imara zaidi. Kuna kitu kilitokea.”
Baadaye, katika hafla ya maombi iliyoandaliwa na kikundi binafsi, alisema, “Ni Mungu aliyeniokoa.”
Rais huyo wa chama cha Republican, ambaye ni Mkristo asiyeegemea dhehebu lolote, aliitaja uhuru wa kidini kuwa “sehemu ya msingi wa maisha ya Marekani” na akaapa kuutetea kwa hali ya juu.