Video za Diddy Zatua Kwa Waendesha Mashtaka
Sakata la staa mkubwa wa muziki duniani, Sean ‘Diddy’ Combs linazidi kufukuta ambapo mashtaka mengine mapya yamefunguliwa dhidi yake, akihusishwa na unyanyasaji wa kijinsia wakati akiendelea kusota katika Gereza la Metropolitan, Brooklyn jijini New York.
Wakati hayo yakiendelea, habari nyingine kubwa kumhusu staa huyo, ni kupatikana kwa video za baadhi ya matukio yaliyokuwa yakitokea kwenye party zake za Freak Off ambapo inaelezwa kuwa mmoja kati ya wafanyakazi wake wa kiume, amewakabidhi waendesha mashtaka ‘mkanda’ wa video za matukio mbalimbali.
Inazidi kuelezwa kuwa, ndani ya video hizo, wanaonekana watu wengine wengi mashuhuri ingawa haijaelezwa wazi ni watu gani wanaoonekana kwenye video hizo.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, mbali na kufika kwenye mikono ya wapelelezi, video za party za Freak Off za Diddy, zimevujishwa pia kwene ‘dark web’, upande wa giza wa intaneti kunakouzwa na kupatikana vitu haramu.
Upande wa pili kuhusu mashtaka mapya, mwanamitindo wa zamani Jane Doe amejitokeza na kueleza kuwa staa huyo aliyeshinda tuzo ya Grammy, alimchanganyia dawa za kulevya kwenye pombe kisha kumbaka na kumpa ujauzito.
Mlalamikaji huyo ameendelea kudai kuwa Diddy alimpa ujauzito na wafuasi wake wakawa wanamshinikiza kutoa ujauzito huo ambao baadaye uliharibika.
Madai hayo yanafanana na yale yaliyotolewa na takriban watu wengine kumi tangu Cassie Ventura, mpenzi wa zamani wa Diddy alipomtuhumu hadharani kwa makosa kama hayo.