The House of Favourite Newspapers

Vifo vya kimbunga Idai kusini mwa Afrika vyaongezeka

 

IDADI ya watu waliopoteza maisha kutokana na kimbunga Idai kilicholikumba eneo la kusini mwa Afrika zaidi ya juma moja lililopita, imeongezeka  ambapo nchini Msumbiji imeongezeka kutoka watu 242 hadi 417, Waziri wa Ardhi na Mazingira nchini humo Celso Correia ameeleza.

 

Idadi hii mpya inafanya waliopoteza maisha Msumbiji, Zimbabwe na Malawi kufikia 700 ambapo idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi.

 

 

Kimbunga kimeua takribani watu 259 nchini Zimbabwe na Malawi 56 wote hao ni kutokana kutokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko.

 

Hata hivyo, Umoja wa Mataifa umesema serikali za nchi hizo zitaweza kutathmini madhara pale maji yatakapopungua kwa mara nyingine.

 

”Tutasubiri mpaka maji yaliyotokana na mafuriko yaishe kisha tutafahamu kwa hakika kuhusu idadi ya waliopoteza maisha nchini Msumbiji, alisema ofisa wa uratibu, Sebastian Stampa.

 

Maelfu ya watu wamenasa sehemu mbalimbali kutokana na mafuriko, ambapo  vituo vingi vya uokoaji vya nchini Msumbuji vimeanza kupokea vyakula.

Watu takriban milioni 1.7 wameathirika kusini mwa Afrika, wakiwa hawana umeme na maji, hasa kwenye maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga hicho.

 

Siku ya Ijumaa, ilielezwa kuwa kumetokea mlipuko wa maradhi ya kipindupindu mjini Beira, katikati mwa Msumbiji.  Shirika la Msalaba mwekundu lilionya hatari ya kutokea maradhi mengine ya mlipuko, huku tayari kukiwa na taarifa ya mlipuko wa maradhi ya malaria.

 

 

Wafanyakazi wa mashirika ya misaada wanawasilisha misaada taratibu wakikabiliwa na changamoto ya kuwafikia wengine walio kwenye maeneo yasiyofikika huku vyombo vya anga vya kupeleka misaada vikielezwa kuwa vichache.

 

Makundi ya watoa misaada nchini Msumbiji yanasema kuwa takriban watu 90,000 wanaishi kwenye maeneo ya muda mfupi huku maelfu wengine bado wakiwa kwenye maeneo yaliyofurika kutokana na mvua, Shirika la Habari la Ufaransa limeripoti.

Comments are closed.