The House of Favourite Newspapers

VIFO VYA WANAHABARI CHANZO CHATAJWA

MSIBA mbichi ni wa mwanahabari nguli nchini, Ephraim Samson Kibonde (47) ambaye alifariki dunia ghafla Machi 7, mwaka huu na kuongeza orodha ya vifo vya wanatasnia hiyo vilivyoacha mshtuko na maswali mengi juu ya vyanzo vyake.  

 

Akiwa kwenye mazishi ya bosi wake ambaye ni Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba (49), kampuni anayofanyia kazi Kibonde akiwa mwenye afya njema, ghafla aliwaambia wafanyakazi wenzake waliokuwa karibu yake pale kaburini: “Ninajisikia vibaya.”

 

Kauli hiyo ya Kibonde ndiyo ilikuwa mwanzo wa safari yake ya kurudi mavumbini alikotokea na kwamba hata madaktari walipojitahidi kumundolea hali ya kujisikia vibaya, haikuwezekana. Wanahabari wengine walioanza safari kwa “kujisikia vibaya” ni Sarah Dumba ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Njombe na Elizabeth Mayemba wa Gazeti la Majira.

 

Mwingine ambaye kifo chake kilishtua wengi ni Glory Mziray, Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), ambaye baada ya kumaliza taarifa yake mbele ya wanahabari wenzake, alisema: “Ninajisikia vibaya” na muda mfupi baadaye aliripotiwa kupoteza maisha.

 

Aina hii ya vifo vya “Ninajisikia vibaya” imekuwa msalaba mzito kwa wanahabari wengi kiasi cha kujiuliza nini chanzo cha yote na hatua zipi za kuchukua ili tasnia iepukane na vifo vya aina hiyo miongoni mwa wanahabari.

 

DAKTARI AFUNGUKA

Daktari maarufu nchini Godfrey Chale hivi karibuni alipoulizwa na mwandishi wa habari hii chanzo cha vifo vya ghafla na kutolewa mfano wa mtangazaji wa Redio DW ya Ujerumani ambaye ni Mtanzania, Isaack Muyenjwa Gamba aliyefariki dunia ghafla usingizini alisema: “Kwanza niwatoe hofu wanahabari kuhusu matukio ya vifo vya ghafla, hili si jambo linalowakuta wao peke yao, ni la watu wote.

 

“Maana nimesikia mengi tangu Kibonde afariki dunia, waandishi wengine wamekuwa na hofu kwamba huenda kuna hujuma za kisayansi. “Lakini ukweli mambo yanayochangia vifo vya ghafla yako mengi, mfano ulaji vyakula usiofaa, unene kupita kiasi, kutokufanya mazoezi, magonjwa ya moyo na kisukari.

 

“Matatizo katika mishipa ya damu, ulevi kupindukia, uvutaji wa sigara mambo haya yote yanachangia vifo vya ghafla.” Aliongeza kuwa ili watu waepukane na matatizo ya aina hiyo wanatakiwa kufuatilia maendeleo ya afya zao na kuchukua hatua za ushauri watakazopewa na wataalam wa afya.

 

DAKTARI BINGWA WA MOYO ANENA

Akizungumza hivi karibuni, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo, alisema tatizo la mishipa kuziba na kuleta madhara makubwa kwa mgonjwa linazidi kuongezeka hasa katika nchi zinazoendelea.

 

“Mshipa wa damu ukiziba husababisha mtu kupata mshtuko wa moyo na inapotokea hali hiyo mtu akiwa usingizini, hufariki dunia,” alisema. Alisema zipo sababu hatarishi nyingi zinazochangia kuziba kwa mishipa ya damu, ikiwamo ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, unywaji pombe kupita kiasi, uvutaji sigara, uzito mkubwa na kutokufanya mazoezi.

 

Dk Pallangyo alisema kiwango cha mafuta kikiwa kikubwa katika damu kuliko inavyotakiwa, huenda kuziba mishipa ya damu na kwamba athari huanza kuonekana mtu anapofikisha umri wa miaka 40 hadi 45. “Lakini kadiri miaka inavyokwenda mbele, tatizo linazidi kujitokeza zaidi katika kundi la vijana, hapa JKCI kwa siku tunachunguza kati ya watu watatu hadi watano kujua kama wana tatizo hili.

 

“Kwa wiki tunaona wagonjwa wapatao 35 ambao ukikadiria kwa mwezi ni kati ya wagonjwa 140. Mwaka 2015/16 tuliwachunguza takriban watu 400 katika mtambo wetu maalum wa ‘Cath Lab’,” alisema. Daktari huyo alisema asilimia 45 kati ya watu hao waliochunguzwa afya zao, walikutwa mishipa yao imeziba hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji.

 

WENGINE WAONYWA

Aidha, Dk Chale aliwatahadharisha waandishi wengine kuwa makini na afya zao kwa sababu taifa linawategemea katika kuleta mageuzi ya kiuchumi.

“Pamoja na kwamba vifo vinapangwa na Mungu, lakini sisi kama binadamu tunayo nafasi kubwa ya kuamua kuhusu afya ya miili yetu. “Mtu kama unakunywa pombe kupita kiasi halafu huli chakula kizuri au unavuta sigara ni wazi kwamba unajiweka kwenye hatari ya kufa mapema na wakati mwingine ghafla, tofauti na mtu anayeepukana na tabia hatarishi za kiafya.

 

“Nenda kwenye nchi za wenzetu, mfano Japani, watu wako makini sana na suala la afya ndiyo maana kwao kuwa na mtu mwenye miaka 100 na siyo ishu, lakini hapa kwetu miaka 60 umekuwa mlima mrefu wa watu kupanda.

 

VIFO VYA WANAHABARI VILIVYOTIKISA

Baadhi ya vifo vya wanahabari vilivyotikisa ni pamoja na cha Glory, Ruge, Sarah, Kibonde, Gamba na Elizabeth.

Wengine ni Nana Mollel aliyewahi kufanya kazi katika Kituo cha Televisheni cha ITV na Radio One cha jijini Dar na Raymond Kaminyonge wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

 

MAYAGE MAYAGE

Mwanahabari mkongwe na mahiri Mayage Mayage aliyekuwa mhariri Gazeti Raia Tanzania alifariki dunia Desemba 25, 2017 na msiba wake kuwahuzunisha wengi.

 

SAGATI, NGAYOMA

Aliyekuwa Ofisa Habari wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Shadrack Sagati alifariki dunia kwa ajali ya ya gari wakati akiwa katika majukumu yake ya kazi huku John Ngayoma aliyekuwa akifanya kazi Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), akifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

 

HALIMA MCHUKA, MISANYA BINGI

Mtangazaji nguli wa kike wa mpira wa miguu, Halima Mchuka aliywahi kufanya kazi Redio Tanzania na Misanya Bingi aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wao walipoteza maisha baada ya kupata mshituko na kupooza.

MWENYEZI MUNGU AZIWEKE ROHO ZA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI NA ATUJALIYE SISI TULIO HAI MWISHO MWEMA WA MAISHA YETU – AMINA.

Comments are closed.