ALIYEKUWA Makamu wa Rais wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Acacia, Deo Mwanyika na Mshauri wa Serikali ndani ya Kampuni hiyo, Alex Lugendo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka 39, yakiwemo ya utakatishaji fedha, kughushi na kula njama.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kevin Mhina na Jopo la mawakili watatu wakiongozwa na wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, Wakili Jackilline Nyantori na Shadrack Kimaro.
Mbali na Mwanyika na Lugendo, washtakiwa wengine ni kampuni ya Mgodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu ambao wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, mashtaka saba ya yakughushi, mashtaka 17 ya Utakatishaji wa fedha, shtaka moja la kuwasilisha nyaraka za uongo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzanian (TRA), shtaka moja la kuongoza uhalifu wa kupangwa, mashtaka 8 ya kukwepa kodi na shtaka moja la kutoa rushwa.
Wakili Nchimbi amedai washtakiwa hao pamoja na wengine ambao bado hawajakamatwa, walitenda makosa hayo kati ya Aprili 11, 2008 na Juni 30, 2008 katika sehemu tofauti za jiji la Dar es Salaam, Kahama Mkoani Shinyanga, Tarime Mara, Biharamulo Kagera maeneo ambayo yapo katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo katika mji wa Johannesburg, Afrika Kusini, Toronto Canada na nchini Uingereza ambapo imedaiwa katika kipindi hicho, washtakiwa hao walikula njama ya ya kutenda makosa ya kughushi na ukwepaji wa kodi. Pia mshtakiwa Mwanyika (56), na Lugendo (46), wanadaiwa kutoa msaada katika kusimamia mkakati wa kihalifu kwa nia ya kupata faida.
Washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Mei 16.2008 na Desemba 31,2008 huko Kahama na Biaramulo, walitoa tamko la uongo kwa kamishna Generali wa TRA kwa nia ya kukwepa kulipa kodi ya USD 9,309,600 ambayo ilikuwa ni kodi iliyopaswa kulipwa kwa TRA.
Washtakiwa Mwanyika na Lugendo wanadaiwa kati ya Desemba 2009 na Desemba 31 2018, ndani na nje ya Tanzania walisaidia mgodi wa North Mara kuhamisha fedha kiasi cha USD 374,243,943,45 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la makosa ya kughushi na kukwepa kodi.
Wanadaiwa kati ya Novemba 2, 2012 na Novemba 27, 2015 huko Shinyanga walitoa Rushwa ya Sh. 718,520,001.76 kwa Hussein Kashindye ambaye ni mkuu wa upelelezi makosa ya jinai wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kumshawishi ili aweze kuachana na uchunguzi wa makosa ya jinai yaliyokuwa yametendwa na Mgodi wa Bulyanhulu.
Washtakiwa hao wakiwa na nia ya ulaghai waligushi mkataba wa mkopo wakitaka kuonyesha kwamba Aprili 30, 2014 Kampuni ya Pangea Limited ilikubali kukopa USD 90,000,000 ikiwa na riba kutoka Benki ya Kimataifa ya Barrick huku wakijua kuwa siyo kweli.
Mshtakiwa Mwanyika anadaiwa Aprili 30, 2018, BOT iliyopo wilaya ya Ilala, kwa makusudi aliwasilisha nyaraka ya uongo ya mkopo baina ya Kampuni Mgodi wa Bulyanhulu na Barrick International Bank Corp kwa madhumuni ya kuonesha kuwa, kati ya June 2001 na Desemba 13.2007 Bulyanhulu walijipatia mkopo usio na faida wa USD 416,100,000 kutoka Barrick.
Washtakiwa hao hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika. Na kesi itatajwa tena Oktoba 31, mwaka huu.
Comments are closed.