The House of Favourite Newspapers

Vigogo Simba Wavamia Nyumbani Kwa Kibwana

0

IMEELEZWA kuwa vigogo watatu wa Simba wamevamia nyumbani kwa beki wa pembeni wa Yanga, Kibwana Shomari eneo la Bigwa wilaya ya Morogoro Mjini, kwa lengo la kuishawishi familia hiyo ili beki huyo asiongeze mkataba na Yanga kisha asaini Simba.

 

Kibwana alijiunga na Yanga Agosti 9, 2020 kwa mkataba wa miaka miwili ambapo kwa sasa anatumikia msimu wake wa mwisho katika mkataba huo aliojiunga na Yanga akitokea Mtibwa Sugar.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, dada wa kwanza wa mchezaji huyo ambaye anafahamika kwa majina ya Zubeda Shomari, aliweka wazi kuwa uongozi wa Simba ulifika nyumbani kwao siku ya Jumanne ya Novemba 2 ambapo kubwa ambalo walilihitaji kutoka kwao ni kumshawishi beki huyo kutoongeza mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Yanga ili wamsajili wao Simba.

“Ni kweli siku ya Jumanne viongozi wa Simba watatu ambao siwafahamu kwa majina yao walikuja na gari aina ya Prado nyumbani kwetu ambapo walinikuta mimi na mama yangu na walipojitambulisha kuwa ni viongozi wa Simba waliomba kuongea na mama yangu ambaye pia ni mama wa Kibwana Shomari.“

 

Walipomaliza kuongea na mama wakaondoka kisha mama akaniita akaniambia kila kitu huku kubwa zaidi walimuomba mama amshawishi Kibwana asiongeze mkataba wake wa kuendelea kuichezea Yanga kwa kuwa mkataba wake unakaribia kumalizika ndani ya Yanga.

 

“Na walimuambia kama atakubali kusaini Simba, wao watampatia mshahara mkubwa, watamjengea nyumba kubwa ya kifahari na kumnunulia gari kwa kuwa wao ni timu kubwa na yenye uhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa,” alisema Zubeda Shomari.

 

Kibwana Shomari kwa sasa amekuwa katika kiwango bora ndani ya Yanga ambapo mara baada ya ujio wa beki Djuma Shabani ambaye anacheza katika nafasi ya beki wa kulia, Kibwana amehamishiwa upande wa kushoto ambapo amekuwa akicheza vizuri pia na kitendo ambacho kimesababisha aitwe
kwenye timu ya taifa, Taifa Stars.

 

Championi Ijumaa liliwasaka viongozi wa Simba jana mchana, likianza na Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, ambaye alisema apigiwe baadaye lakini alipotafutwa simu yake haikuwa ikipokelewa.

 

Jitihada za gazeti hili zilitua kwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori lakini naye simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa. Jitihada zitaendelea kufanyika ili kusikia upande wa Simba wanasemaje.

Marco Mzumbe, Dar es Salaam

KESI ya MBOWE: VURUGU ZAIBUKA MAHAKAMANI, WAFUASI wa MBOWE Wafungiwa NDANI…

Leave A Reply