The House of Favourite Newspapers

Vigogo wafurika kwa Sangoma kumdhibiti Magufuli

0

IMG_2480
Mtabili maalim Hassan Yahya Hussein.

Gladness Mallya na Hamida Hassan, RISASI MCHANGANYIKO
DAR ES SALAAM: Kasi ya utumbuaji majipu ya Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ inazidi kuwatisha watendaji wengi wabadhilifu, wababaishaji na wazembe serikalini kiasi kwamba, baadhi yao wamekuwa wakipigana vikumbo kutafuta kinga kwa namna nyingi, ikiwemo kwenda kwa waganga wa kienyeji ‘sangoma’ na watabiri.

JIUNGE NA RISASI MCHANGANYIKO
Gazeti hili lilipata taarifa kutoka kwa vyanzo vyake kuhusu namna ya baadhi ya vigogo kumiminika kwa waganga wa kienyeji na watabiri kwa lengo la ‘kupikwa’ ili wasinaswe katika anga za Rais Magufuli, ambaye amekuwa hana simile kwa watumishi wa umma wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi zao.

IMG_2481Akiongea na mwandishi wetu.

MSIKIE MTABIRI MAALIM HASSAN YAHYA HUSSEIN
Maalim Hassan Yahya Hussein, mtoto wa mtabiri maarufu wa zamani, marehemu Yahya Hussein, ambaye watu wengi humuita ‘sangoma’ wakimfananisha na waganga wa kienyeji licha ya kuwa mnajimu, alifikiwa na gazeti hili nyumbani kwake, Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam na kuulizwa kuhusu ukweli wa taarifa hizo ambapo bila ajizi alikiri kuwepo kwa suala hilo.

“Ni kweli, vigogo wengi wa nyadhifa kubwakubwa wamekuwa wakija kwangu kutaka niwatabirie kama wako katika orodha ya kutumbuliwa majipu na Rais Magufuli ili waweze kujiandaa mapema.
“Wanataka niwape dawa ya kumdhibiti Magufuli asiwafikie kitu ambacho si kazi yangu kwani mimi ni mnajimu.”

YEYE ANATAZAMIA NYOTA TU
“Mimi huwa nawatazamia nyota zao, siogopi kuwaambia ukweli maana utabiri ndiyo kazi yangu na huwa ninaangalia nyota, siyo kwamba natunga au natoa kichwani mwangu. Wengi wakishajua ukweli wanajikuta wakihaha maana rais wetu hana mchezo nao,” alisema maalim Hassan.

KINA NANI HAO?
Risasi Mchanganyiko lilipenda kuwajua kwa majina baadhi ya vigogo hao ambao wameshafika nyumbani kwa maalim ili kushughulikiwa, lakini mtabiri huyo alikataa katakata kuwataja, akisema maadili ya kazi yake hayaruhusu hata mara moja kutoa siri za wateja wake, ingawa alisisitiza ni wengi na wenye nyadhifa kubwa serikalini.

TANGA NAKO
Vyanzo vingine vimeanika kwamba, baadhi ya vigogo serikalini wamekuwa wakienda mkoani Tanga kwa mganga mmoja wa kienyeji na kukesha huko wakikingwa na utumbuaji wa majipu unaofanywa na JPM.
Mmoja anayetajwa kukesha kwa mganga jijini Tanga ni bosi wa shirika kubwa la umma ambaye aliendeshwa na dereva wake mpaka mkoani humo na kufanyiwa ‘madongoloji’.

Magufuli3Rais John Pombe Magufuli.

HOFU YAZIDI KUTANDA
Hofu kubwa imetanda kwa watendaji wa ngazi za juu katika idara mbalimbali za serikali kufuatia kusimamishwa kazi kwa mabosi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ambao wanadaiwa kutumia vibaya kiasi cha shilingi bilioni 180.

Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba bado kuna idara nyingi za serikali ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kutokana na utendaji wake dhaifu, lakini zikiwa na matumizi makubwa ya fedha.

WENGI WAMETUMBULIWA
Mbali na vigogo wa Nida, Dk. Magufuli pamoja na mawaziri wake wameshatumbua majipu tofauti katika sekta mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Leave A Reply