VIJANA WA UMRI CHINI YA MIAKA 25 HATARINI KUAMBUKIZWA VVU

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Emil Kasigara (kulia) akizindua rasmi Jukwaa la “SITETELEKI” litakalozungumzia masuala ya afya hususani vijana walio chini ya umri wa miaka 25 ili waweze kujitambua na kuwa na tabia chanya.  Uzinduzi huo ulifanyika mwishoni mwa wiki katika Hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza.

 

UWEZEKANO wa vijana walio chini ya umri wa miaka 15 hadi 24 kushindwa kutimiza ndoto zao za maisha ni mkubwa endapo hawatapata elimu sahihi ya afya ya uzazi na maambukizi ya Ukimwi (VVU) itakayowasaidia kufanya maamuzi sahihi kwa mstakabali wa maisha yao.

 

Mtaalamu wa Masuala ya Afya kutoka Wizara ya Afya, Gerald Kihwele, akiwakilisha mada ya “SITETELEKI” kwa wadau wa afya (hawapo pichani).

Kundi hilo liko kwenye hatari hiyo kutokana na kukabiliwa na changamoto za ongezeko la maambukizi mapya ya VVU na mimba za utotoni kwa sababu ya uelewa mdogo (elimu) na upungufu wa huduma rafiki za afya ya uzazi na VVU kwa vijana.


Akizindua Jukwaa la Vijana ( SITETEREKI Najifunza Kila Hatua),  Kaimu Katibu Tawala wa Msaidizi Mkoa wa Mwanza, Emily Kasigara, alisema serikali kupitia Wizara ya Afya wakishirikiana na Mradi wa USAIDI Tulonge Afya fhi 360 imeanzisha jukwaa hilo la vijana ili kuwajengea uwezo katika masuala ya afya ya uzazi na Ukimwi, wajitambue na kubadilisha tabia zao.

Alisema serikali, jamii na wadau wana kazi kubwa ya kuwaelimisha vijana kujitambua, wakijitambua na kujali afya
zao kutakuwa na matokeo chanya kwao na watafanya maamuzi sahihi, hawatachezea afya zao na kuwahimiza waende vituo vya huduma za uzazi na kupima afya.

“Jukwaa la SITETEREKI Najifunza Kila Hatua litakuwa kimbilio la vijana kufikia maisha wanayoyahitaji kwani ni eneo muhimu ambalo ni nguvu kazi na taifa la kesho, watapata mahali pa kutoa dukuduku zao na watajengewa uwezo.  Lengo la serikali ni wafikiwe ili wasijiingize kwenye changamoto zinazowaharibu na kuhatarisha maisha yao ya baadaye,”alisema Kasigara.

Alisema serikali imeanzisha jukwaa hilo litakalowawezesha kuwa na maisha bora baada ya kujengewa uwezo na kujitambua watatimiza azma ya serikali ya Tanzania ya uchumi wa kati wa viwanda kwani familia ikiwa duni kiafya haitakuwa na mchango kwenye uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake Mratibu wa Elimu Afya ya Uzazi Wizara ya Afya Dk. Gerald Kihwele alisema licha vijana kuwa tegemeo kiuchumi wanakabiliwa na changamoto nyingi ambapo vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 sawa na asilimia 40 wana maambukizi ya VVU, kati ya hao asilimia 70 ni wasichana na ndio wanaokabiliwa na hatari ya maambukizi mapya.

Alisema ni asilimia 41 tu ya vijana wa kiume wanaozingatia njia za afya ya uzazi na wanatumia kinga kwa usahihi wakati wa kujamiiana huku wasichana wanaopata huduma hizo wakiwa ni asilimia 37 na ndio wenye changamoto kubwa hivyo wakijengewa uwezo watajitambua na kusimama kwenye misimimo thabiti.

Dk. Kihwele alieleza kuwa serikali inafanya jitihada kubwa za kuweka mazingira bora ya huduma ya afya ya uzazi kwa vijana na kuwafanya wawe sehemu ya mipango yake, hivyo lazima kuwe na huduma za viwango vya kuwavutia na kuchochea fikra zao waende kwenye maeneo ya kutolea huduma.

“Upatikanaji wa huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana bado si za kuridhisha ni asilimia 30 hivyo hatuwezi kuwavutia vijana waende kupata huduma hizo ambapo serikali zifikie asilimia 80 na ipo haja mitizamo ya watoa huduma ivutie na kuhamasisha vijana wazichangamkie,”alisema Dk. Kihwele.

Naye Mshauri Mwandamizi wa SBCC Shahada Kinyanga alisema vijana hupewa taarifa zisizo sahihi na wanakosa motisha ya kufikia malengo yao kimaisha hivyo jukwaa la SITETEREKI litajibu changamoto zao na kuibua hisia za kufikia matarajio na mahitaji yao, litawaongezea ukweli kabla ya kujiingiza kwenye uhusiano na kufanya uamuzi sahihi.

“Tunalenga maeneo yatakayonyesha mafaikio makubwa katika kuboresha afya za vijana wa Kitanzania wa umri wa miaka 15 hadi 24 hasa huduma za afya ya uzazi kabla ya ujauzito, upimaji wa VVU na tohara ya hiari kwa wanaume. Baadaye tutahusisha vipaumbele vya jamii na kimaisha kwani takwimu zinaonyesha VVU na mimba za utotoni husababisha afya duni na vifo kwa vijana,” alisema Kinyanga.

Alisema jukwaa hilo ambalo lipo chini ya Wizara ya Afya, ndani ya mradi wa miaka mitano wa USAID Tulonge
Afya wanalenga kuwafikia vijana 22,800 kwa mwezi kwa kuwatumia wahamasishaji 520 katika Kanda ya Ziwa na
Magharibi na kati ya wahamasishaji hao 270 ni wasichana.

Toa comment