The House of Favourite Newspapers

Vijana Wapigwa Msasa Kuhusu Masuala ya Amani

0
Mmoja wa wakilishi kutoka Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, Inspekta Danford Mahundu akizungumza na vijana ambao ni mabalozi wa Amani wilayani Tandahimba mkoani Mtwara.

SHIRIKA la Global Peace Foundation Tanzania kupitia mradi wa ‘Vijana Katika Ujenzi wa Amani’ limetoa mafunzo kwa vijana wa mkoa wa Mtwara wilaya ya Tandahimba kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa Amani.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mikakati ya shirika hilo kuwafunda vijana wa mipakani namna ya kuilinda, kuithamini na kuitunza amani nchini.

Mradi huo uliopewa jina la Youth Action for Peace (YAP), unafanyika katika wilaya nne za mkoa wa Mtwara kwa kuwajengea uwezo makundi mbalimbali ndani ya jamii mkoa huo kwa lengo la kuidumisha amani.

Ofisa tawala wilaya ya Tandahimba, Francis Mkuti akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo.

Akifungua warsha ya vijana katika ujenzi wa amani wilayani Tandahimba kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, Kanali Patrick Sawala; Katibu tawala, Juvenile Jaka Mwambi ametoa wito kwa vijana kuondokana na dhana potofu za kutumia kivuli cha dini kuvuruga amani nchini.

 

Mbali na kuipongeza Global Peace Foundation kwa kuanzisha mradi huo kwa wilaya hiyo ya mipakani, Mwambi amesema makundi ya vijana kama vile waendesha bodaboda na wengine waliolengwa kufikiwa katika mradi huo, ni makundi sahihi katika mradi huo.

Amesema vijana wengi wa mikoa na wilaya ya mipakani wamekuwa wakilaghaiwa na makundi ya watu wasio na nia njema kwa jamii hivyo mafunzo haya ni ya muhimu sana kwa Vijana wetu wa Tandahimba.

Katibu tawala wilaya ya Tandahimba, Juvenile Jaka Mwambi akizungumza katika mafunzo hayo kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo.

Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa makundi mbalimbali ya kijamii kama vile viongozi wa dini, wazee wa vijiji na kimila, wazazi, walezi, walimu na wadau wengine kuwa mabalozi wema wa kuhubiri amani ili nchi iendelee kuwa na utulivu kwa maendeleo ya Taifa.

Aidha, Mkurugenzi Mkazi wa Global Peace, Martha Nghambi amesema mradi huo wa YAP ambao umefadhiliwa na Jukwaa la kimataifa la masuala ya kuzuia ukatili – IDOVE, unatarajiwa kutekelezwa kwa muda wa mwaka mmoja hapa nchini.

Jukwaa hilo la IDOVE lilianzishwa mwaka 2017 kwa ushirikiano wa pamoja na Tume ya Umoja wa Afrika, Kurugenzi ya Wananchi na Mashirika ya Diaspora (AUC-CIDO) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Mkurugenzi Mkazi wa Global Peace, Martha Nghambi (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo.

Pamoja na mambo mengine amesema wamepanga kuyatumia makundi hayo maalumu kwa lengo la kuwaelimisha vijana umuhimu wa kuitunza, kulinda na kuepuka vishawishi vyovyote vinavyoweza kuivuruga amani nchini.

Kwa upande wake, Mmoja wa wakilishi kutoka Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, Inspekta Danford Mahundu alitoa wito kwa vijana wilayani humo kuwafichua watu au makundi ya vijana yanayojihusisha na masuala ya uvunjifu wa Amani, alisisitiza kuwa Jeshi la Polish lipo tayari kushirikiana na wana nchi katika maswala ya ulinzi na Usalama.

Aidha, Mwenyekiti wa walemavu wa ngozi wilayani Tandahimba, Rashid Yusph Mchangi amesema walemavu ni mojawapo ya makundi yanayoathiriwa pakubwa pindi amani inatopoweka hivyo ni vema jamii kushirikiana kuelimisha vijana umuhimu wa kuitunza Amani.

Warsha hiyo ilihudhuriwa pia na viongozi wa dini akiwamo Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tandahimba, Thomas Ambwange na Imam wa Msikiti wa Tandahimba, Irasha’s Mtepa pamoja na wadau wengine.

Aidha, Ofisa tawala wilaya ya Tandahimba, Francis Mkuti aliyefunga warsha hiyo mbali na kuwapongeza vijana hao kwa utayari wao kuwa mabalozi wa Amani kupitia Shirika la Global Peace Foundation Tanzania, pia aliahidi ofisi ya mkuu wa wilaya kuwa ipo tayari kufanya nao kazi.

NA MWANDISHI WETU

Leave A Reply