The House of Favourite Newspapers

VILABU 6 UINGEREZA VYAMSAKA SAMATTA

MSHAMBULIAJI nyota wa mabingwa wa ligi ya Ubelgiji, klabu ya Genk na nahodha wa ttmu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta, huenda akatua Ligi Kuu ya England (Premier) msimu ujao.

Samatta, maarufu kama Samagoal, amedokeza kuwa kuna vilabu sita vya Ligi ya Premier ambavyo vinapigana vikumbo kumsajili.

 

“Kwa sasa sipo katika nafasi nzuri ya kuelezea ni klabu gani lakini pia kuna klabu nyingine mbili kutoka Hispania ambazo zimekuwa zikiisaka saini yangu. Hata hivyo, mimi ndoto zangu ni kucheza katika Ligi Kuu ya England,” amesema Samatta.

Hii si mara ya kwanza kwa Samatta kuhusishwa na uhamisho wa kwenda Ligi ya Premier, lakini inaonekana kuwa safari hii mambo yameiva.

 

“Ndiyo, nitaondoka mwishoni mwa msimu huu…(klabu ya England) moja inanifukuzia sana na imekuwa ikipiga simu kwa wakala wangu kila siku,” amesema Samatta.

 

Katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari mwaka huu, klabu ya Cardiff ilituma ofa ya Pauni milioni 13 kumng’oa Genk, lakini uhamisho huo ukakwama.  Hata hivyo, Cardiff imeshuka daraja.

 

Ukiachana na Cardiff, vyombo vya habari vya Uingereza mwaka jana viliripoti klabu nyingine tatu za nchini humo ambazo zilikuwa zikihusishwa na kutaka huduma ya ushambuliaji kutoka kwa Samatta. Klabu hizo ni Everton, Westham na Burnley.

Kipenzi cha mashabiki Genk

Samatta ameendelea kuwa kipenzi cha mashabiki wa Genk msimu huu baada ya kuongoza safu ya ushambulizi wa timu hiyo na kunyakua ubingwa wa ligi hiyo baada ya kuukosa kwa miaka minane. Straika huyo mwenye miaka 26, ameifungia Genk magoli 23 na kumaliza kama mshambuliaji bora wa ligi. Pia ameifungia magoli tisa kwenye michuano ya ligi ya Europa.

 

Jina la Samatta limekuwa likiimbwa na mashabiki wa Genk, na wamekuwa wakimuomba mshambuliaji huyo kusalia klabuni hapo kucheza ligi ya Mabingwa Ulaya. Samatta ameiambia Mwananchi kuwa moyo wake upo England japokuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Mabingwa ni kitu cha kutamanisha pia.

 

Hata akihamia England, bado atakuwa ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kufanya hivyo. Pia amekuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi ya Europa.

“Hawa jamaa (Genk) hawajacheza Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2011 enzi za akina (Kevin) De Bruyne, najua wanataka nicheze msimu ujao lakini Ligi Kuu ya England ina heshima yake…ni ligi ambayo tayari imepiga hatua kubwa sana kulinganisha na Ligi Kuu ya Ubelgiji. Ni ligi ambayo inapendwa na watu wengi duniani, Ligi inayoonekana sehemu kubwa duniani. Yaani kwa vitu vingi iko mbali.”

 

Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016 ambapo alitia saini mkataba wa kumweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20. Amebakiwa na miezi 12 kabla ya mkataba wake kumalizika.

 

Samatta alihamia Ubelgiji mwaka mmoja baada ya kutawazwa mchezaji bora wa mwaka Mwafrika aliyekuwa anacheza ligi za barani Afrika mwaka 2015. Alishinda vikombe sita vikuu akiwa na TP Mazembe ikiwa ni pamoja na kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2015 kabla ya kuondoka. Samatta aliichezea Simba kabla ya kujiunga na TP Mazembe mnamo mwaka wa 2011.

Comments are closed.