Vingine Mnashea, kwa nini simu iwe tatizo?
NAPENDA kumshukuru Mungu kwa kila jambo katika maisha yangu ya kila siku kwani ni kwa rehema zake tu ndizo zinanifanya nakutana nawe msomaji wangu.
Leo nitazungumzia jambo ambalo wapenzi wengi wamekuwa wakilichukulia mzaha na kuliona la kawaida lakini kiukweli ni la kukemea sana. Hivi inawezekanaje mkashea penzi na vitu vingine lakini kwenye kuchangia simu iwe tatizo?
Binafsi naona hapo kuna tatizo kubwa sana, tatizo ambalo ukijiuliza mara mbilimbili utagundua linaongozwa na usaliti wa chinichini wa wapenzi husika.
Siku zote imezoeleka kuwa mwanamke na mwanaume wanapoamua kuishi pamoja ni kama wameungana na kuwa kitu kimoja, ndiyo maana shuka yao ni moja. Wanakula chakula pamoja, wanafanya mambo mengi pamoja lakini kwa nini kwenye kushea simu kuwe na tatizo?
Usiri huo ni wa nini? Kama siyo kudhihirisha kuwa wewe ni mchepukaji na kwenye simu yako kumejaa madudu yako kisa mwenzio hashiki simu yako ni
nini sababu ya kufanya hivyo?
Ni dhahiri kabisa kuwa kizazi hiki kimetawaliwa na jinamizi la uasherati. Haiwezekani simu ya mwenza wako iwe siri kiasi hicho, la hasha! Kuna jambo ndani limejificha.
Hilo ni janga, inasikitisha! Haileti mantiki kwa wapenzi wawili wenye mapenzi ya dhati, uaminifu na wanataka kujenga familia bora kufichana kilichomo ndani ya simu.
Nini kinakufanya mpenzi wako, mumeo, mkeo asishike simu yako, tena ukiona anaelekea kwenye kugusa sehemu ya picha (gallery) mamaaa…! ndiyo unampokonya kabisa mkeo simu yako na kumtupia maneno makali; “Nani kakuambia ushike simu yangu, unatafuta nini huko. Kila mtu ashike simu yake, mambo ya kusachi vitu vyangu sitaki.’’ Hapo kama mwanaume hataki mkewe ashike simu na mwanamke hataki mumewe au mpenzi wake aguse simu yake unategemea nini?
Si inaonesha kabisa kuwa kizazi hiki cha ‘dot com’ kimejaa usaliti. Ukiona mpenzi wako hataki kushika simu yake basi ujue hilo ni jipu tena jipu uchungu ambalo halihitaji hata kusubiri liive ili litumbuliwe, wewe libonyezebonyeze tu utaujua ukweli.
Karibu kwa maoni yako kuhusu mada hii na yatatoka wiki ijayo kwenye kona hii
Kwa ushauri na maoni tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Ista:mimi_na_ uhusiano au jiunge kwenye group letu la WhtsApp kwa namba iliyopo juu.