The House of Favourite Newspapers

Viongozi 18 Watimka ACT Wazalendo, Polepole Adai CCM Itatawala Milele

SAKATA la kuhama hama vyama vya siasa hapa nchini bado linaendelea ambapo viongozi 18 wa chama cha ACT Wazalendo kutoka mikoa mbalimbali nchini wamejivua nyadhifa zao na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM.

 

Shughuli ya kuwapokea wanachama hao wapya limefanyika jana Januari 17, 2018 Mjini Moshi na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ambaye pia amejiunga CCM hivi karibuni akitokea ACT.

 

Akitoa hotuba fupi baada ya kupokea wanachama hao, Polepole amesema katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano, CCM imeongeza wanachama zaidi ya milioni mbili na kwa mwendo huo basi chama hicho huenda kikatawala nchi milele.

 

Tukisimamia haki na heshima kwa watu wote CCM itatawala milele nchi hii. Kwa sababu misingi ya chama hiki ni utu. Sasa tunahitaji watu ambao wanachukizwa na rushwa, ubadhirifu na ubinafsi,”amesema Polepole.

 

Miongoni mwa wanachama hao, wapo waliokuwa wajumbe wa kamati kuu, wenyeviti wa mikoa na makatibu wa ACT Wazalendo ambao wameeleza sababu za kukihama ACT Wazalendo ni kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya viongozi waandamizi wa chama hicho akiwemo RC Mghwira  kuhamia CCM.

 

Baadhi ya majina ya viongozi  wa ACT Wazalendo waliohama ni Eva Kaka (mjumbe  Kamati Kuu),  mwenyekiti wa Mkoa wa Dodoma Anganile Massawe, Athuman Balozi (mwenyekiti mkoa wa Tabora), Hamad Nkya (mwenyekiti mkoa wa Kilimanjaro), Godwin Kayoka (katibu wa mkoa Tabora) na Juma Hamisi (mwenyekiti wazee mkoa wa Singida).

Comments are closed.