visa

VIPODOZI NUSURA VIMUUE MFANYABIASHARA, ASIMULIA!

DAR ES SALAAM: IDADI ya watu wanaotumia vipo­dozi hapa nchini na hasa wanawake ni kubwa na tahadhari imekuwa ikitolewa uchwao kwamba, baadhi vina madhara. 

 

Sikio la kufa halisikii dawa! Meza za kina dada wengi zimefurika vipodozi vya kila aina, lengo ni kutafuta urembo ambao wengine umewaweka matatizoni kama mfanyabi­ashara maarufu wa vipodozi nchini Elizabeth Kalili ‘Grace Zoazoa.’ Je, mchimba shimo kaingia mwenyewe?

 

Kwamba mu­uza vipodozi vimemdhuru mwenyewe? Jibu linatolewa na mwanamke huyo alipo­fanya mahojiano na gazeti hili hivi karibuni. “Nilikuwa nimebobea kwenye matumizi ya vipodozi kwa ajili ya kujichibua ili niwe mweupe.

 

“Nilikuwa sichagui kipo­dozi cha kutumia kwenye ngozi yangu. Kuna wakati sura yangu na ngozi yangu ilikuwa haieleweki, kumbe vipodozi vingine nilikuwa na­tumia vyenye sumu,” alisema Elizabeth. Aliongeza kuwa zoazoa yake ya vipodozi haiku­muacha salama kwani ali­jikuta akiambulia magonjwa ya ngozi ambayo baadaye yalikuja kugeuka na kuwa kansa ambayo ilitishia uhai wake.

“Nilivyoona ngozi yangu inakuwa mbaya na kuharibi­ka niliacha kutumia, ikabidi niende Muhimbili (Hospitali ya Taifa) kutokana na mata­tizo niliyoyapata. “Ilibidi madaktari wani­fanyie upasuaji mdogo ambao baadaye waliniambia kuwa nina kansa,” alisema. Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa majibu hayo yalimuogopesha na kum­fanya ajutie matumizi ya vipozi ambavyo madaktari walimwambia kuwa baadhi vilikuwa na sumu.

 

Hata baada ya kupata mkasa huo mzito mwan­amke huyo hakukaa kimya na kusubiri afe bali alijikuta akihangaika huku na kule kupigania uzima wake. “Kuhangaika huko ndiko kulikonifikisha kwenye utafiti na tiba ya ngozi kupitia matunda, nilijifunza mengi kupitia vitabu na wataalamu mbalimbali huku majaribio ya tiba zangu yakiwa ni mwili wangu. “Huwezi amini baada ya muda ile hali ya ngozi kutoeleweka rangi ilitoweka, nikaanza kuona dalili njema.

 

“Baadaye nikaamua kwenda Hospitali ya Apollo iliyopo nchini India, lengo likiwa ni kuhakiki afya yangu, wataalam waliponipima wakasema sina kansa, nikamshukuru Mungu sana,” alisema Elizabeth. Mfanyabiashara huyo anawashauri wanawake wenzake kuwa makini na matumizi holela ya vipodozi, badala yake wazingatie vile ambavyo vimethibitishwa kitaalam.

“Vipodozi vya asili ni vizuri kwa sababu havina kemikali hatari, mimi vimenisaidia na kunitoa katika hatari ya kifo,” alisema. Pengine swali la msingi, ni wanawake wangapi ambao wako makini kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam wa tiba ya ngozi hasa matumizi yasiyo sahihi ya vipodozi vilivyopigwa marufuku?

 

Bila shaka wengi bado wameziba pamba masikio yao na kuendelea kuwa kokoro la vipodozi mbalim­bali, hata vile vilivyopigwa marufuku na hivyo kujiweka katika hatari ya kupatwa na msemo huu wa “Usiposikia la mkuu utavunjika guu,” wenye maana kuwa, wak­iendelea kupuuza ushauri unaotolewa wanavunjika guu kwa kupata magonjwa ya ngozi ikiwemo kansa.
Toa comment