Viporo vya Magufuli Baraza la Mawaziri siri yafichuka

magufuli_aapaRais John Pombe Magufuli.

Mwandishi wetu
Nyuma ya viporo vinne vilivyoachwa kwenye Baraza la Mawaziri la Rais John Pombe Magufuli bila majina ya mawaziri wake, vinadaiwa kubeba siri nzito ambayo imefichuka.

Wizara nne ambazo Rais Magufuli aliziacha wazi juzi, wakati wa kutangaza baraza hilo kwa maelezo kwamba hajapata majina ni pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi.

Wizara hizo aliziacha chini ya manaibu waziri ambapo Wizara ya Fedha na Mipango naibu wake ni Dk. Ashanti Kijachi, Wizara ya Maliasili na Utalii alimuweka naibu wake awe ni Ramo Makani, Naibu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alimtaja Edwin Ngonyani na Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi alimweka Stella Manyanya.

Duru za kisiasa zimenyetisha kuwa, Rais Magufuli alifikia hatua ya kuziacha nafasi hizo wazi baada ya wahusika waliokuwa wakipewa taarifa za uteuzi wao kuomba waachwe kulingana na wizara zenyewe walizotajiwa wataziongoza.

“Kwa utendaji wa Magufuli, kila aliyekuwa akitajiwa wizara mojawapo kati ya hizo, aliomba aachwe kwani wizara hizo nne zinaonekana ni mfupa mgumu na kwamba jamaa (Magufuli) anazitolea macho mno.

“Kwa hiyo ili kukwepa lawama au kufukuzwa kazi kama rais alivyosema kwamba wasifanye sherehe za kuteuliwa na badala yake wajiandae kufanya sherehe za kufukuzwa, kila mmoja akaona uwaziri kwenye wizara hizo ni sawa na gunia la misumari.

“Wewe fikiria wizara kama Maliasili na Utalii ilivyo na changamoto zake hasa mambo ya ujangili na upotevu wa mapato, kwa namna jamaa (Magufuli) alivyo, hawezi kushuhudia mambo kama hayo yakitokea ‘so’ mtu anayepewa nafasi hiyo lazima awe amejipanga vilivyo.

“Wizara nyingine ni hii ya Fedha na Mipango. Magufuli bwana ni mtu wa kubana matumizi na hataki masihara kwenye masuala ya mapato na matumizi. Sasa kila aliyeambiwa atateuliwa kuwa waziri wake aliomba asiteuliwe hivyo rais anaendelea kutafuta mtu sahihi,” kilisema chanzo chetu ndani ya Serikali ya Rais Magufuli na kuongeza:

“Ndivyo ilivyokuwa kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi kwani kila aliyeambiwa anateuliwa aliomba asiteuliwe kwa kuhofia kutimuliwa au kugombana na mheshimiwa (Magufuli) kwani hashindwi kwenda wizarani kisha akaondoka na kiti cha waziri.”

Kwa upande wao wanachi waliozungumza na gazeti hili walimpongeza Rais Magufuli kwa kuteua baraza dogo lenye wizara 18, mawaziri 19 tu na baadhi ya wizara kuwa na manaibu waziri na nyingine zikiwa hazina huku akifuta semina elekezi.

Wizara alizounda na mawaziri wake kwenye mabano ni Wizara ya Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora (George Simbachawene na Angela Kairuki), Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira (Januari Makamba) na Wizara ya Ajira, Walemavu (Jenista Mhagama).

Nyingine ni Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Mwigulu Nchemba), Nishati na Madini (Prof. Sospeter Muhongo), Katiba na Sheria (Harisson Mwakyembe), Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Augustino Mahiga), Ulinzi na Kujenga Taifa (Hussein Mwinyi), Mambo ya Ndani (Charles Kitwanga), Ardhi na Maendeleo ya Makazi (Wiliam Lukuvi), Viwanda na Biashara (Charles Mwijage), Afya, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii (Ummy Mwalimu), Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo (Nape Nnauye) na Wizara ya Maji na Umwagiliaji (Makame Mbarawa).

 


Loading...

Toa comment