HALI ya hewa ya joto la Dar es Salaam imeonekana kuwatesa AS Vita wanaocheza na Simba leo usiku. Juzi walisitisha mazoezi mara tatu ili kupumzika na kunywa maji.
AS Vita leo watakuwa wageni wa Simba katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Taifa saa 1 Usiku, mshindi atakwea moja kwa moja hatua ya robo fainali.
Championi ambalo lilihudhuria mazoezi ya kwanza ya Vita juzi Alhamisi yaliyoanza saa 9 Alasiri kwenye Uwanja wa Gymkhana ambapo wachezaji walionekana wakivuja jasho muda wote huku wakiomba mapumziko mara kwa mara.
Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwa dakika 97 chini ya Kocha Florent Ibenge na msaidizi wake, Raoul Shungu, wachezaji walionekana kuzidiwa na jua na kusababisha wapumzike mara tatu kwa zaidi ya dakika saba na kwenda kupumzika sehemu yenye kivuli huku wakinywa maji mengi kukata joto.
Hata walipotakiwa kuingia uwanjani kuendelea na mazoezi wachezaji hao walionekana kujivuta muda mwingi wakitamani kuendelea kukaa kwenye kivuli kutokana na jua kuwa kali huku walinzi wa eneo hilo wakigoma kabisa waandishi kuwasogelea.
MARTHA MBOMA
Comments are closed.