Vita ya Kiatu cha Ufungaji Bora Yawaka Moto Ligi Kuu 2024/25
Katika mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25, hali bado ni ya kutabirika kwa ugumu, huku mechi chache zilizobaki zikiwa na nafasi ya kubadilisha kila kitu.
Kwa sasa, Jean Ahoua wa Simba SC anaongoza akiwa na mabao 16. Anafuatiwa kwa karibu na washambuliaji wawili wa Yanga SC – Clement Mzize na Prince Dube – wote wakiwa na mabao 13. Hata hivyo, Dube anakabiliwa na maumivu yaliyopunguza kasi yake, jambo linalomwacha Mzize kuwa tegemeo pekee kwa Yanga kwenye mbio hizi.
Simba SC pia ina nguvu nyingine kupitia Leonel Ateba, ambaye amefikisha mabao 13, akiwapa matumaini mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi endapo Ahoua atateleza.
Mchezaji mwingine anayefanya vizuri ni Jonathan Sowah wa Singida Black Stars, licha ya kujiunga dirisha dogo. Amefunga mabao 12 katika kipindi kifupi, huku timu yake ikibakiwa na mchezo mmoja dhidi ya Tanzania Prisons unaotarajiwa Juni 22, 2025.
Kwa upande wa Yanga SC na Simba SC, kila moja inabakiwa na mechi mbili tu – dakika 180 muhimu zitakazotoa picha halisi ya nani atang’ara na kiatu cha dhahabu msimu huu.
Pacome wa Yanga naye anasalia kuwa mchezaji wa kuangaliwa, akiwa na mabao 11 na kiwango bora.
Vita hii ya wafungaji ni ya kuvutia kwani kila mchezaji ana ndoto ya kuhitimisha msimu kwa heshima binafsi. Itakuwaje? Tusubiri dakika za mwisho kuamua.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, mtunzi wa kitabu Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo.
Kupata nakala: Piga simu 0756 028 371.
Kinapatikana pia Njombe – Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni – Tupokigwe, na Posta karibu na Mnara wa Askari kuelekea IFM.
Kazi mpya: Moyo Wangu Unavuja Damu – itazinduliwa rasmi Julai 24, 2025. Usipange kukosa!