Vodacom Kusambaza Shangwe Na Kugusa Maisha Msimu Huu Wa Sikukuu
Msimu wa sikukuu ukiwa unakaribia, kampuni ya Vodacom Tanzania imezindua kampeni inayojulikana kama ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’ yenye lengo la kuwazawadia wateja wake zawadi mbalimbali pamoja na kutoa bima ya afya kwa mama na mtoto Tanzania bara na visiwani Zanzibar.
Akizungumza wakati wa kuzindua kampeni hiyo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Tanzania, Bi. Linda Riwa amebainisha kuwa msimu huu wa sikukuu utakuwa wa kipekee kwa sababu, mbali na kuendesha promosheni zinazolenga kuwazawadia wateja wa Vodcom pia watatoa bima ya afya kwa watoto watakaozaliwa mwezi wa Disemba 2023 pamoja na mama zao.
“Sambaza Shangwe, Gusa Maisha – kama jina la kampeni linavyojieleza, inalenga kusambaza shangwe na kugusa maisha ya wateja wetu pamoja na jamii nchini kote. Kuhakikisha wateja wanabakia na tabasamu na kuwa katika hali ya shamrashamra tunapoelekea kufunga mwaka, tutakuwa tutaendesha droo za wiki ambapo wateja wenye bahati watajishindia zawadi mbali mbali ikiwemo pesa taslimu mpaka kiasi cha shilingi milioni kumi, bodaboda, luninga, simu janja, routers za 5G na 4G na nyinginezo nyingi.
Ninaamini zawadi hizi sio tu zitaacha tabasamu miongoni mwa wateja wetu bali pia zinaweza kubadili maisha yao endapo zitatumika katika shughuli za kiuchumi na hivyo kuwaongezea kipato,” alisema Bi. Riwa.
Kampeni ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’ iliyozinduliwa leo inatarajiwa kudumu kwa takribani wiki 10 mpaka katikati ya mwezi Januari 2024, ambapo kwa mwezi Novemba kampeni hii itajikita katika kuwazawadia na kuwakabidhi wateja zawadi mbalimbali, na mwezi Disemba itatumika mahususi kwa kutoa zawadi ya upendo ya bima kubwa ya afya kwa mama na mtoto.
“Kwa kuongezea, Vodacom itagusa maisha katika jamii kupitia zawadi ya upendo ya bima kubwa ya afya ya mwaka mmoja tutakayoitoa kupitia bidhaa yetu ya VodaBima. Bima hii itatolewa kwa watoto watakaozaliwa ndani ya mwezi Disemba kwani tunajali kesho ya kizazi hiki kijacho.
Lengo letu ni kuwapatia wazazi utulivu wa akili katika malezi ya mwaka wa awali wa watoto wao ambao ni wa msingi sana katika ukuaji wa mtoto hivyo kuhakikisha changamoto za kiafya zinashughulikiwa ipasavyo. Kwa hili napenda kuwashukuru sana wateja wa Vodacom kwani wao ndio wanatuwezesha kugusa maisha ya watoto hawa pamoja na familia zao,” aliongezea Bi. Riwa.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa M-Pesa, Bw. Epimack Mbeteni ameongezea kuwa Vodacom inatambua kuwa katika msimu huu wa sikukuu Watanzania wengi hufanya manunuzi na malipo ya huduma mbalimbali hivyo Vodacom inawahimiza kufanya miamala hiyo kupitia njia za kidigitali haswa M-Pesa kwani ni rahisi na salama zaidi. Vile vile, kadri wateja wanavyofanya miamala kwa njia hii ndivyo wanavyojiongezea nafasi ya kujishindia zawadi za papo kwa hapo au zile zitakazotolewa kupitia droo za kila wiki.
Kwa kumalizia, Mkurugenzi wa Huduma za Kidijitali Bw. Nguvu Kamando alifafanua kuwa “tunaelewa katika msimu huu wa sikukuu, kuwasiliana na wapendwa wetu ni moja kati ya vipaumbele vyetu hivyo basi, kila mteja atakapofanya manunuzi ya muda wa maongezi au bando kupitia menyu kuu ya *149*01# au kupitia M-Pesa atajiongezea nafasi za kushinda zawadi kemkem.
Naomba nitoe msisitizo ili kujiongezea nafasi ya kushinda wateja wanahimizwa kufanya manunuzi haya kupitia M-Pesa kwa kupiga *150*00# au kupitia aplikesheni ya M-Pesa. Kama hiyo haitoshi, wateja wataingia kwenye droo pale wanapopakua aplikesheni ya Mdundo DJ mixes.”