The House of Favourite Newspapers

Vodacom wazindua Mtandao Supa

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania PLC, Hisham Hendi (Katikati) Akizungumza na waandishi wa Habari

Kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi inayoongoza Tanzania Vodacom Tanzania PLC leo imezindua kampeni yake ya Mtandao Supa yenye lengo la kuongeza ufahamu kwa wateja kuhusu mtandao wake wenye ubora wa hali ya juu na manufaa makubwa yanayopatikana kwa wateja wake katika mtandao huu supa wa Vodacom. (Super Vodacom network)

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania PLC, Hisham Hendi alisema Vodacom imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuboresha miundo mbinu ya mawasiliano katika miaka iliyopita kwa ajili ya kuhakikisha upatikanaji wa mtandao katika maeneo ya mijini na vijijini nchini.

“Jitihada za kampuni ya Vodacom Tanzania kuhakikisha kwamba Tanzania nzima imeunganishwa na inadhihirishwa kupitia uwekezaji wetu na mikakati yetu ya upanuzi wa upatikanaji wa huduma.

“Kuna wastani wa vituo kumi vya sauti na data vinavyojengwa, kupanuliwa au kuboreshwa katika siku moja kwa lengo la kutoa huduma ya uhakika na ubora wa hali ya juu kwa wateja wetu. Huu ni ushahidi katika jitihada zetu za kuhakikisha kwamba tunatoa huduma bora kwa wateja wetu. Tumewekeza zaidi ya shilingi bilioni 171.4 kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mtandao wa 4G katika miji mikubwa na kuboresha kiwango cha ubora wa mtandao wetu katika jitihada za kubadilisha maisha ya Watanzania kupitia technolojia.” Alisema bwana Hendi.

Bwana Hisham anawahimiza watu wengi zaidi wanufaike na huduma hii ya kiwango cha juu kilichoko katika ofa kwa madhumuni ya kuboresha maisha yao kupitia teknolojia katika maeneo ya elimu, huduma kwa njia ya mtandao, biashara na burudani.

“Tunaamini katika nguvu ya teknolojia katika kubadilisha maisha ya jamii na kuleta mabadiliko chanya kwa watu binafsi, taasisi, biashara na sekta kama vile elimu ya afya na huduma za serikali kupitia mtandao,” alihitimisha bwana Hisham.

Imeandaliwa na Neema Adrian/GPL

 

 

 

 

 

Comments are closed.