VYAKULA KWA WENYE KISUKARI WAKATI WA MFUNGO

MWEZI Mtukufu wa Ramadhani unaendelea, waislamu wote duniani wapo katika mfungo huu, ibada ambayo pamoja na mambo mengine inawataka wafunge kwa kutokula chakula kuanzia asubuhi na kufungulia (kufuturu) jioni.  Hata hivyo, kuna watu wanaishi na kisukari na wanafunga, au wengine ni wagonjwa wa kisukari na wanatamani sana kushiriki katika hii ibada ila wanajiuliza watawezaje kufunga ilhali wanaishi na kisukari.

Muislamu yeyote au Mkristo mwenye rafiki Muislamu mwenye tatizo hili atafaidika na makala haya kwani tutaelekeza nini cha kufanya ili mfungaji mwenye ugonjwa huu asipate madhara ya kiafya.

Yafuatayo ni mambo kadhaa muhimu sana ya kuzingatia kwa wenye kisukari wakiwa ndani ya mfungo na maisha baada ya mwezi wa Ramadhani. Ya kufanya ni haya: Mosi, mshirikishe daktari wako kabla hujaamua kufunga na hata kama umefunga ni muhimu kushauriana naye, ufanye vipimo vyote vya sukari ili kujua kama hali yako na kiwango chako cha sukari kinaruhusu kufunga. Hakikisha ulijiweka tayari kwa mfungo miezi mitatu au minne kabla ya mfungo kuanza na ulifuata mfumo sahihi wa ulaji bora wa vyakula kwa wenye kisukari.

Pili; hakikisha kama ulifanya mazoezi na kutumia dawa kama ulivyoshauri na daktari (kama u-mtumiaji wa dawa za kisukari.)

Tatu; kama kuna maradhi yanayotokana na kisukari, kama vile ugonjwa wa moyo, figo, ganzi miguuni na kadhalika, daktari atakupima kuangalia kiwango cha sukari yako kwenye damu na atakushauri nini cha kufanya, baada ya hapo daktari ataweza kukushauri jinsi ya kula kulingana na majibu ya vipimo vyako.

Pia, ni muhimu kuzingatia ushauri wa daktari, kama majibu ya vipimo vinaonyesha unaweza kufunga au ukifunga kutasababisha hatari, kwa mfano sukari inaweza kushuka au kupanda sana na kusababisha matatizo makubwa, zingatia ushauri huo.

Ikitokea wakati wa kufunga siku moja ukapoteza fahamu ni vyema ukamuona daktari haraka akakupima kiwango chako cha sukari na ukafuata ushauri wake ambao atakupa. Wakati wa kufuturu ni muhimu kuzingatia ulaji sahihi wa mwenye kisukari, mara nyingi futari inahusisha aina mbalimbali ya vyakula na vingi huwa ni vya wanga na huwekwa sukari, kuwa makini sana wakati wa kufuturu, baada ya hapo pima kiwango cha sukari yako kwenye damu.

Wakati wa kufuturu epuka kabisa kunywa uji hata kama uji huo hauna sukari, epuka pia kula aina za kunde kama vile maharage au kunde zilizotiwa sukari. Mara zote chagua aina ya futari ambayo haitapandisha sukari yako, kwa mfano upawa mmoja wa muhogo, kachumbari au mboga za majani na chai isiyo na sukari inaweza kuwa ya maziwa inafaa. Nimeshasema kwamba usitumie uji kwa sababu ni wanga; muhogo pia ni wanga ni rahisi kupandisha sukari yako mwilini.

Ni bora kula viazi vitamu (mbatata) kuliko muhogo lakini navyo visizidi vipande viwili, au tumia ndizi mbichi zilizochemshwa kwa chai au maziwa pia mkate uwe wa brown au mchele wa brown, kumbuka mboga za majani na matunda hasa tikiti maji, korosho, karanga ni muhimu sana katika futari yako, jiepushe na nyama au vyakula vya mafuta mengi.


Loading...

Toa comment