VYAKULA VYA MGONJWA WA KISUKARI AINA YA KWANZA!

KISUKARI ni ugonjwa unaoathiri kongosho. Wakati wa uzalishaji wa insulini huwa haizalishwi au mfumo huwa haufanyi kazi vizuri, na ikiwa hali hii haitadhibitiwa, inaweza kusababisha matatizo makubwa kwenye macho, figo, neva, mishipa ya damu, ini na moyo.  Kisukari aina ya kwanza, ambapo insulini inakuwa tegemezi (insulin-dependent); kongosho halitengenezi kabisa insulini au linatengeneza kwa kiasi kidogo sana kiasi kwamba mgonjwa analazimika kuchomwa sindano ya insulini. Aina ya kwanza ya kisukari inaweza kutokea kwa watu kuanzia utotoni mpaka kwa watu wa umri wa miaka 30. Aina hii ya kisukari hushambulia kwa haraka sana.

Kwa kuwa kongosho halifanyi kazi vizuri, usawa wa damu-sukari lazima upewe uangalizi wa karibu. Watu wenye kisukari aina hii ya kwanza pia huwa na uzito pungufu. Ni muhimu kula vyakula vyenye afya unapokuwa na kisukari aina ya kwanza. Hata hivyo, hii haina maana kwamba unalazimika kuacha kila chakula ukipendacho sababu tu una kisukari. Ni muhimu pia kufuatilia kiasi cha damu sukari katika mwili wako kila siku.

Insulini ni sehemu tu ya mambo muhimu ya kuzingatia. Mlo sahihi na kamili pia mazoezi ya viungo vina umuhimu mkubwa kwa mtu mwenye kisukari aina ya kwanza. Unapochagua kula vyakula vyenye afya kila siku vinaweza kukusaidia kuweka sukari katika kiwango kinachotakiwa. Kula mlo sahihi kunaweza pia kukusaidia kuepuka matatizo mengine yahusianayo na kisukari kama ugonjwa wa moyo, magonjwa ya ini na kudhurika kwa neva.

Baadhi ya wataalamu wamekuwa wakifikiri kwamba kuna lishe au chakula maalumu kwa ajili ya mtu mwenye kisukari. Wamekuwa wakidhani kwamba mtu mwenye kisukari hatakiwi kabisa kutumia vyakula au vinywaji vyenye sukari na baadhi ya vyakula. Lakini unapokuwa na kisukari aina ya kwanza unaweza kula vyakula vyovyote vyenye afya kama mtu mwingine yoyote.

Fuata huu muongozo:

Punguza kutumia mafuta yasiyo na afya. Haya ni mafuta yatokanayo na wanyama, maziwa, siagi ya wanyama, nk. Mafuta yasiyo na afya yanaongeza uwezekano kwako wa kupatwa na ugonjwa wa moyo. Unapokuwa na kisukari hatari ya kupata ugonjwa wa moyo inakuwa kubwa zaidi. Hivyo kuwa makini na chaguo la chakula chako ili kupunguza hatari hiyo. Pili; kula vyakula vingi vyenye nyuzinyuzi ambavyo vinaweza kukusaidia kudhibiti sukari yako.

Unaweza kupata nyuzinyuzi toka katika vyakula ambavyo havijakobolewa, maharage, matunda na mboga za majani. Jitahidi upate gramu 25 mpaka 30 kila siku za nyuzinyuzi. Vyakula hivyo vyenye nyuzinyuzi kwa wingi ni bora zaidi kwa mgonjwa wa kisukari aina ya kwanza kuliko vile vyenye nyuzinyuzi chache kama vile vilivyokobolewa na vile vyenye sukari nyingi ya dukani.

KUTAMBUA KIASI CHA WANGA UNACHOKULA

Vyakula vya wanga ndiyo vyakula pekee ambavyo ni chanzo kikuu cha nguvu cha mwili. Unavipata hivyo katika vyakula vingi unavyokula kama mikate, tambi, mboga za majani, matunda, maziwa, viazi, ugali, wali, sukari nk.

Vyakula vya wanga vinapandisha sukari yako kuliko vyakula vingine vyovyote. Kujua ni kiasi gani cha wanga unakula ni namna nzuri ya kudhibiti kisukari. Unaweza kushirikiana na daktari wako au na mtaalamu yoyote wa lishe kufanya hesabu kujua ni kiasi gani cha wanga mwili wako unahitaji kila siku.

Baadhi ya watu hudhani kuwa sukari husababisha kisukari na hivyo mtu mwenye kisukari eti asitumie kabisa sukari. Lakini kisukari aina ya kwanza husababishwa na sababu za kijenetiki na mambo mengine yasiyohusu sukari moja kwa moja. Hata hivyo vyakula vingi vitamu vina wanga mwingi ambao unaweza kuathiri sukari katika damu yako.

Acha kabisa kutumia soda, mafuta ya wanyama na vyakula vya makopo. Pamoja na hayo bado nashauri upendelee kutumia vyakula au vinywaji vyenye nishati kidogo na visiwe vimeongezwa sukari ya kutengenezwa.

Vyakula vifuatavyo vina wanga kidogo na vina viinilishe muhimu kama kalsiamu, potasiamu, nyuzinyuzi, magnesiamu na vitamini zingine muhimu. Vyakula hivyo ni maharage, mboga za majani zenye rangi ya kijani, matunda kama tikiti maji au jamii ya machungwa, viazi vitamu, nyanya, samaki na vyakula ambavyo havijakobolewa. Vyakula vingine ni mbegu za maboga, mtindi usio na mafuta ndani yake, maziwa yasiyo na mafuta.


Loading...

Toa comment