The House of Favourite Newspapers

Vyombo vya Habari Uganda Vyagoma Kurusha Hotuba ya Museveni

0

VYOMBO vya habari binafsi nchini Uganda, vimekataa kurusha hotuba ya Rais Yoweri Museveni ambayo alikuwa amepanga kufanya kila Jumapili, kuanzia saa moja kamili jioni hadi saa tatu usiku saa za Kampala.

 

Museveni alikuwa ameagiza vyombo vyote vya habari nchini Uganda kurusha hotuba yake ya kila wiki, lakini muungano wa wamiliki wa vyombo hivyo umekataa agizo hilo wakisema huu ni msimu wa kampeni na kwamba hawawezi kutoa fursa kwa mgombea mmoja pekee bila kuzingatia wagombea wengine kwa sababu inavunja kanuni za uandishi wa habari.

 

Taarifa ya muungano wa wamiliki wa vyombi vya habari Uganda umeiandikia tume ya mawasiliano Uganda – UCC —  ukisema kwamba “Museveni ni mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu mwa mwaka 2021 na kwa hivyo tukipeperusha hotuba yake, wasikilizaji na watazamaji watachukulia ujumbe wake kama kampeni.”  Hayo yameandikwa na katibu wa muungano huo, Joseph Beyanga.

 

Kulingana na sheria ya utangazaji nchini Uganda ya mwaka 2013, kila mgombea katika uchaguzi anastahili kupewa nafasi sawa katika vipindi na habari zinazochapishwa au kupeperushwa na vyombo vyote vya habari nchini humo. Kulingana na msemaji wa Museveni, Don Wanyama, hotuba ya Museveni ya Jumapili ilikuwa imepangiwa kuangazia usalama na ukuaji wa uchumi.

 

Baada ya muungano wa vyombo vya habari kukataa kupeperusha hotuba hiyo, Wanyama aliandika ujumbe wa twitter kwamba “hotuba ya rais imeahirishwa hadi siku ambayo tutawaarifu. Tunasikitika kwa usmbufu wowote ambao umejitokeza.”

 

“Tungependa kujua aina ya hotuba atakayotoa Rais Museveni kabla ya kupanga namna ya kuipeperusha. Iwapo hotuba hiyo ni kampeni, basi vyombo vya habari vinavyotaka kuipeperushwa vinastahili kulipwa kwanza,” imesema barua ya muungano wa wamiliki wa vyombo vya habari kwa UCC.

 

Maafisa wa UCC hawajajibu barua hiyo. Museveni mwenye umri wa miaka 76, anagombea muhula wa sita kubaki madarakani kupitia chama cha National Resistance Movement (NRM).

 

Machafuko yalitokea Uganda wiki iliyopita baada ya polisi kumkamata mgombea wa urais wa chama cha National Unity Platform – NUP –  Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.

 

Wine alifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya kufanya kampeni katika njia inayoweza kusambaza virusi vya Corona. Aliachiliwa kwa dhamana na anaendelea na kampeni yake.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.

Leave A Reply