WA KUMUOKOA Q CHILLAH NI HUYU!
CHILLAH ambaye jina lake halisi ni Aboubakar Shaban Katwila, ni bonge moja la mwanamuziki mwenye uwezo mzuri wa kuimba. Ana mchango mkubwa kwenye gemu la Bongo Fleva na ana mashabiki wengi wanaofuatilia kazi zake tangu akiwa solo, alipounda Top Band na Khaleed Mohammed ‘T.I.D’ kisha baadaye akawa solo tena hadi leo.
Kuhusu kutangaza kuacha muziki hivi karibuni, hazikuwa habari za kushtua sana kwa wengi ukizingatia si mara ya kwanza kutangaza kufanya hivyo ingawa huko nyuma alidai ‘unga’, ndiyo ulisababisha afikie uamuzi huo, lakini wakati huu ametangaza akiwa hana unga kichwani.
Mbali na hilo la kuacha muziki, kilichoshtua zaidi kwenye tangazo lake la sasa ni kuweka wazi alifikia uamuzi wa yeye kutamani kujiua!
Kiukweli, kwangu ninauchukulia huu kama uamuzi mgumu mno kwa binadamu kuufikia. Nasema kwa sababu sijawahi kuwaza kujiua na ninaamini mtu kufikia mawazo haya ni kwamba ameona hakuna tumaini tena kwenye maisha.
Lakini ninaweza kuipata picha kwa mbali kwa nini Chillah alifikia uamuzi huu. Anaumia, moyo wake unabubujikwa machozi hasa anapotazama mahali alipoutoa muziki wa Bongo Fleva na malipo kiduchu anayoyapata.
Mbali na yote, nimpongeze kwa sababu pamoja na kuwaza jambo hilo baya, hakuweza kulitekeleza. Aliamua kujikaza kiume na kuchukua uamuzi mwingine wa kuachana na muziki.
Hata hivyo, niweke wazi baada ya kumsikiliza akizungumzia masahibu yake ya sasa ‘kaka yangu’ huyu niliwaza kumsaidia. Nikamtafuta, lakini akasema hayupo tayari kuzungumza na waandishi tena kwa sasa kutokana na Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Haikuwa shida, bado kuna njia ya kumsaidia kwa kutumia kalamu yangu na hapa nitamueleza Chillah ukweli na kumuonesha nani anaweza kumsaidia na kumtoa kwenye dimbwi alilozama. Lakini kabla ya kumuonesha mtu huyo, tutibu kwanza ‘saratani’ inayomtafuta.
MUZIKI
Chillah anaamini kwamba muziki ni miongoni mwa sababu za yeye kupoteza tumaini maishani mwake. Kwenye mahojiano aliyoyafanya Mei 15 na mtandao mmoja wa burudani alisema kauli hii; ‘‘How many things gonna I loose because of this music?”
Alikuwa akiuliza swali kwamba ni mambo mangapi atapoteza kwa sababu ya muziki?
Akaweka wazi pia kwamba, mkewe amemkimbia kwa sababu ya kushindwa kufanya vizuri kwenye muziki na kuonekana hana ‘future’.
INAHUZUNISHA
Mke amemkimbia na huo muziki ametangaza kuachana nao. Kuhusu nini atafanya baada ya hapo, hafahamu!
Kaka naomba nikwambie kwamba hata vitabu vya dini vinatupa moyo kwamba kila changamoto ina jawabu lake. Muziki unaweza kuwa kitu kinachokupa
‘stress’ ya muda mrefu, lakini umekwishakaa na kumlilia muumba wako akakupa majibu?
Nimekusikia mara kadhaa ukitoa lawama kwa wadau wa muziki kama Ruge Mutahaba, watangazaji wa muziki na wengine wengi kwamba ni miongoni mwa watu wanaokukwamisha.
Lakini vipi kuhusu wewe mwen-yewe? Unaelewa ni kwa namna gani unajikwamisha kwenye muziki? Umeshawaza juu ya hili? Umeshawaza juu ya ngoma unazotoa zinaendana na muda na soko la muziki la sasa?
Mbona kama ni wadau wa muziki bado wapo wanaokupenda, QS Muhonda alikupa nafasi, mkaenda hadi Nigeria na Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya kazi, lakini bado ‘mzizi’ wa kuitibu saratani ya muziki kwa upande wako haukupatikana!
Mbali na kulaumu, Chillah ni muhimu kufahamu kwamba wakati mwingine tunafikiri matatizo tuliyonayo maishani yanasababishwa na watu fulani. Tunasahau kwamba sisi wenyewe tunaweza kuwa sababu ya matatizo yetu. Lakini nikukumbushe pia, anayekupandisha ndiye atakayekushusha. Kwa hiyo usitegemee zaidi watu kuliko uwezo wako binafsi.
MAPITO
Hili pia ni suala ambalo linamtesa Chillah. Mapito yake ya kutumia unga. Anaamini kwamba watu wanamhukumu kutokana na mapito hayo bila kusahau kwamba kwa sasa yeye anahitaji mtu wa kumwambia; “Chillah ulikosea, upo kwenye njia sahihi na tusonge mbele!”
Ni kweli unahitaji mtu wa namna hii, lakini niamini Chillah, hata asipopatikana, bado unaweza kusonga mbele. Sikwambii urudi kwenye muziki au uachane nao moja kwa moja kama ulivyoamua. Lakini kumbuka kuhama kwenye nyumba uliyoizoea na kuishi ugenini si jambo dogo. Ushauri wangu, unaweza kuendelea na muziki na ukafanya mishemishe zako nyingine, ikiwa tu ukiamua kujikubali wewe kama wewe hata kama hakuna anayekuzungumzia vizuri.
HUYU ANAWEZA KUKUSAIDIA
Mtu wa kukusaidia Chillah ni wewe mwenyewe. Kuwa wa kwanza kujipa moyo, kujitia ujasiri, kuamini kila kitu kinawezekana na wakati huu mgumu unaokumbana nao, unaweza kuupita na kuendelea na maisha mapya.
Kumbuka ngoma yako ya Dreamer na ujumbe ulioutoa.
Kuna sehemu uliimba; ‘Tangu mdogo nilikuwa na ndoto, niishi kitajiri kama John Kaboko, hata mbuyu ulianza kama mchicha, mabonde naamini yatakwisha…’
Uzuri wa maisha ni kuanza ulipo na kuwa na mwisho mzuri hata kama mwanzo wako ulikuwa mbaya kiasi gani. Usikate tamaa, wewe bado kijana, jembe, pambana kwa ajili yako, kwa ajili ya watoto wako na yule unayempenda. Binafsi ninakuombea.
Ramadhan Kareem to you Chillah!
BONIPHACE NGUMIJE
Comments are closed.