The House of Favourite Newspapers

Wa kutuvusha hapa unamjua, usifanye kosa Jumapili!

0

magufuli alivyoomba kura kwa wakazi wa Buchosa kwenye mkutano uliofanyika Nyehunge, mkoani MwanzaMgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Pombe Magufuli

IMEBAKI siku moja tu kabla hatujaamka kuelekea vituoni kwenda kumaliza kazi baada ya miezi kadhaa ya tambo, ahadi, kejeli, vituko na mafigisufigisu mengine ya uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015.

Tumeshuhudia mambo mengi yakiendelea wakati wa kampeni kutoka kwa wagombea wa vyama vyote, ingawa mvutano mkubwa zaidi ulikuwa baina ya John Pombe Magufuli wa CCM na Edward Ngoyai Lowassa wa Chadema, anayeungwa mkono na vyama vinne vinavyounda umoja wa Ukawa.

lowassaaMgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Ngoyai Lowassa.

Ni fursa nyingine adimu, ambayo Watanzania kwa ujumla wao, wanatakiwa kuitumia ili kuweka mizani sawa juu ya mustakabali wa nchi yao, kwani ni wao ndiyo wataamua nani awe kiongozi wao mkuu na hivyo kusubiri kwa miaka mingine mitano kuona kama walifanya sahihi au la.

Ni siku ambayo kosa moja, linazaa matatizo mengi yatakayowaumiza kuanzia wao, familia zao, jamii na mwishowe Tanzania nzima. Huenda tayari umeshaamua juu ya nani atachukua kura yako. Ni sawa, lakini haina ubaya kama utapitia upya kujua kama umefanya uamuzi sahihi au la.

Ili kujua kama uko sahihi au la, kitu cha msingi kabisa kuzingatia ni mahitaji yako. Unajua mahitaji yako ni nini ambayo rais, mbunge na diwani unayeenda kumchagua atayasimamia? Maana wapo baadhi ya wenzetu hawajui wanachokitaka, wao ni kama bendera kufuata upepo, hawana msimamo. Upepo ukigeukia huku nao wapo, ukipinda kona wapo!

Usiwe bendera fuata upepo, kuwa na msimamo na watu wanaokuzunguka wauelewe. Usiogope kumpigia kura mgombea unayemuamini kwa sababu wote ni Watanzania na kupishana mawazo ni jambo la kawaida. Asikutishe mtu, kura ni yako na umpe unayemtaka.

Kama wewe hujui mahitaji yako, mimi yangu nayajua na nitajaribu kukudokeza ili ujue kwa nini kura yangu itaenda kwa mgombea ninayemuamini.

Ninayo ajira lakini ambayo haikidhi mahitaji yangu na familia yangu. Najua hakuna kiongozi atakayenijaza fedha mifukoni, lakini namhitaji mtu ambaye ataboresha upatikanaji wa mahitaji muhimu ya binadamu, kama afya, elimu, chakula, makazi na miundombinu.

Fedha za kuyafanya haya yote zipo, isipokuwa kuna watumishi serikalini ni wezi. Wanaiba pesa zilizopaswa kufanya kazi hiyo. Kuna watu wanaingia mikataba isiyoisaidia nchi, lakini wao wanafaidika. Hawa wanaitwa mafisadi.

Ili nipate huduma bora za kijamii kama nilivyozitaja pale juu, ni lazima wezi na wapiga dili wote waondolewe serikalini, ikibidi wafungwe vifungo virefu. Kwa maana hiyo, kura yangu ya urais itakwenda kwa mtu ninayeamini atasimamia haya kwa dhati.

Hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kuendelea na kuwasaidia wananchi wake kwa serikali yake kujaza ‘vishoka’. Na marais wote waliozifanya nchi zao ziwe na maendeleo ya kuonekana, walikuwa wakisimamia mambo haya!

Unapoitaja China kuwa ndilo taifa linalotishia nafasi ya Marekani kiuchumi duniani, unazungumzia nchi ambayo wala rushwa na mafisadi adhabu yao ni kunyongwa. Hawaangaliani usoni, hata uwe na nafasi gani, ukipatikana na hatia ya mambo hayo, historia yako inaishia hapo.

Kwa kuwa ningependa kuiona Tanzania inayoachwa nyuma na Rwanda kiuchumi ikirejea kileleni kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati kwa kuanzia, naamini nahitaji rais mtendaji, asiye mwoga na asiyezungukwa na marafiki wenye kutia mashaka.

Nchi yetu ina kila kitu, lakini tumekosa mtu msimamiaji. Ili twende sawa, tunamhitaji jemedari mmoja mwenye uchungu na nchi kama Nyerere, lakini mchapakazi asiye mwoga kama Sokoine. Mtu huyo yupo na wewe unamjua, mpe kura yako Jumapili hii!

MUNGU IBARIKI TANZANIA!

Leave A Reply