The House of Favourite Newspapers

Waamuzi ligi kuu walia njaa, TFF, Bodi ya Ligi watofautiana

WAKATI michuano ya Ligi Kuu Bara ikielekea ukingoni huku ushindani ukiongezeka kwa timu zote zinazoshiriki ligi hiyo, mambo huenda yakaenda ndivyo sivyo baada ya baadhi ya waamuzi kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania kupitia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuwalipa stahiki zao wanazodai.

 

Waamuzi hao wamesema endapo watashindwa kufanya hivyo, basi TFF ijiandae kukabiliana na michezo michafu ambayo inaweza kutokea katika ligi hiyo.

 

Wakizungumza na Championi Ijumaa kwa sharti la kutotajwa majina yao, waamuzi hao wamedai kuwa tangu kuanza kwa raundi ya pili katika mzunguko wa 20 wa msimu huu, hawajalipwa fedha zao ambazo hupaswa kupewa baada ya mechi wanazochezesha na kila wanapodai wamekuwa wakipigwa kalenda.

 

“Imefika wakati sasa hata fedha za kutupeleka kwenye vituo vyetu kwa ajili ya kuchezesha mechi tunajitegemea wenyewe, lakini jambo la kushangaza ni kwamba tunapomaliza kuchezesha mechi husika tunapewa fomu za kusaini ambazo zinaonyesha kuwa tumelipwa wakati hatujalipwa.

 

“Kusema kweli jambo hilo linatukosesha amani na kutuacha na maswali mengi kuhusina na madai yetu hayo kama tutalipwa au la, lakini pia linaweza kusababisha tukaanza kujihusisha na vitendo vichafu ili tu tuweze kupata fedha za kujikimu,” walisema waamuzi hao.

 

Championi lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama, kuzungumzia jambo hilo, ambapo alisema: “Taarifa hizo za madai hayo ya waamuzi ninazo, ni kweli kabisa kuna baadhi yao bado hawajalipwa kwa sababu hatukuwa na mdhamini, lakini mtu anayeweza kulizungumzia vizuri suala hilo ni mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi.

 

“Ukimpata anaweza kulizungumzia vizuri hilo, kwa sababu ligi kuu inaendeshwa na bodi hiyo na wao ndiyo wanawalipa waamuzi hao, kwa hiyo wao wanalijua vizuri hilo, ila ninachojua hii changamoto ya kucheleweshewa malipo yao ipo kwa sababu ya kutokuwa na mdhamini.

 

“Mtu anaweza kuchezesha mechi leo na akachelewa kulipwa lakini wakati tulipokuwa na mdhamini walikuwa wanalipwa haki zao, hata hivyo kwa wale ambao hajalipwa naamini kabisa kabla ya ligi kumalizika kila mtu anayedai atakuwa amelipwa.” Alipoulizwa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Boniface Wambura kuhusu hilo, alisema: “Hakuna kitu kama hicho, taarifa hizo hazina ukweli wowote.”

Comments are closed.