The House of Favourite Newspapers

Waamuzi Msisubiri Mechi ya Simba, Yanga Ndiyo Muwe Makini

0

MSIMU wa 2020/21 upo mwishoni, na kuna michuano mingi ambayo inaelekea ukingoni.

 

Hivi karibuni tumeshuhudia timu za Mbeya City na Ihefu zikiamka na kuwa kwenye kiwango kizuri kwa kupata matokeo ya ushindi na lengo lao ni kuukimbia mstari wa kushuka daraja, lakini siyo timu hizo pekee, zipo nyingine nazo zimekuwa zikitoa ushindani mkubwa kwa ajili ya kubakia kwenye ligi hiyo msimu ujao.

 

Hili limekuwa likiifanya ligi izidi kuchangamka na ushindani mkali, lakini wakati ligi ikiwa inanoga na ushindani ukiongezeka, kuna kitu kinaingia katikati yake na kutaka kuharibu utamu wote.

 

Kumekuwa kukidaiwa kuwa kuna maamuzi yasiyo mazuri na yenye kuminya haki yanataka kuharibu juhudi za wale ambao wanavuja jasho uwanjani kuzipambania timu zao. Hii siyo sawa hata kidogo.

 

Kumeanza kuibuka malalamiko kadhaa, mfano baada ya mchezo wa Tanzania Prisons dhidi ya Yanga kuna kauli tata zilitolewa na upande wa timu ambayo ilipoteza mchezo huo na kuanza kuzua sintofahamu.

 

Haipendezi kila siku kitu kinachozungumzwa ni kilekile bila ya kuwa na mabadiliko hata kidogo, haipendezi hali hii kwa sababu kama itadumu kwa muda mrefu inaweza kuja kusababisha maafa hasa kwa wale ambao wanaona wanaonewa na kuminywa kwa haki yao.

 

Haki ifatwe na yule ambaye anatakiwa kuipata basi aipate bila ya kuangalia ni mdogo au mkubwa. Tunaamini ikiwa hivyo basi ligi itakuwa tamu na yenye ushindani.

 

Inawezekana labda kwa kuwa malalamiko yanatolewa katika michezo ambayo inaonekana ni ‘midogo’ au haina nguvu ya kushawishi mambo yazungumzwe, lakini tukumbuke kuwa wikiendi ijayo kuna mchezo ambao unatarajiwa kuteka hisia za wengi, hayo tunayoyasema hapa yasipofanyiwa kazi, mambo yanaweza kuwa mabaya siku hiyo.

 

Hatutaki kuunga mkono uvunjifu wa sheria lakini katika mazingira ya kawaida, tunatoa angalizo kuwa mchezo wa Simba na Yanga ni mkubwa na presha yake ni kubwa.

 

Kama maamuzi hayatakuwa ya kuzingatia kanuni za soka, basi inaweza kuwa mwanzo wa kutengeneza ‘bomu’ lenye madhara makubwa. Waamuzi wenyewe wajitafakari, pia mamlaka zinazohusika katika kusimamia zinatakiwa zichukue hatua mapema.

Leave A Reply