Waandaaji Kili Marathon Washauri Washiriki Kutumia Fursa ya Muda wa Punguzo

Waandaaji wa mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2024 wamewakumbusha washiriki kuwa wamebakiza siku chache tu ambazo ni chini ya mwezi mmoja kunufaika na muda wa punguzo za bei ya usajili iwapo watajiandikisha kabla ya Desemba 12, 2024.
Taarifa iliyotolewa na waandaji wa mbio hizo maarufu Barani Afrika imesema dirisha linalotoa unafuu wa ada ya ushiriki bado liko wazi ambapo pia washiriki wameaswa kujiandikisha mapema ili kuepuka adha ya mrundikano wa dakika za mwisho au kukosa kabisa fursa ya punguzo hizo.
“Kipindi cha washiriki kunufaika na punguzo maaraufu kama ‘ndege alewahi’ kilianza tarehe Oktoba, 21 mwaka huu, ambapo kinatarajiwa kumalizika usiku wa manane Desemba 12, mwaka huu”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza, baada ya hapo ada ya kujisajili itaongozeka kuanzia Desemba 13, 2024, hadi Februari 3, 2025, usiku wa manane au pale tiketi zitakapomalizika, ambapo huduma itatolewa kwa atakaefika kwanza kuhudumiwa kwanza na kwamba nafasi ni chache hivyo ni vyema kila anayetarajia kushiriki akawahi mapema.
Taarifa ya waandaaji hao iliendelea kusema kuwa washiriki wanaweza kujiandikisha kupitia huduma za kifedha za mtandao wa Tigopesa kwa kupiga *150*01#, na kisha kubonyeza 5 LKS, halafu kubonyeza 5 (Tiketi) na kufuata maelekezo ya kukamilisha usajili au kupitia tovuti rasmi ya www.kilimanjaromarathon.com na kwamba swala hilo ni kwa washiriki wa vipengele vyote vya 42km, 21 km na 5km.
“Hii inatumika kwa makundi yote ya mbio zikiwemo Kilimanjaro Premium Lager 42 KM (Full Marathon), kilomita 21 (Tigo Kili half marathon) na 5Km Fun Run,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa usajili unapaswa kufungwa kabla ya Februari 23, 2025 na kwamba wakati toleo la 23 la mbio hizo linatarajiwa kufanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), ili kuhakikisha tukio hilo linaambatana na kanuni rasmi za shirikisho la riadha la kimataifa (IAAF) zinazohusiana na idadi ya washiriki ili kuhakikisha usalama wa washiriki wakati wa tukio hilo.
“Lengo la kuzingatia kanuni hizo za IAAF ni kuhakikisha washiriki wanafurahia muda wao wakati wa suhiriki wa mbio hizo kwa kuepuka msongamano mkubwa na wakati huo huo kuhakikisha huduma zingine kama vile za vituo vya maji na huduma za afya zinatayarishwa kulingana na idadi ya washiriki”, ilisema taarifa hiyo.
Kilimanjaro Premium Lager ndio wadhamini wakuu wa mbio za marathon na imeshika nafasi hiyo ya udhamini mkuu tangu kuanzishwa kwa mbio hizo miaka 23 iliyopita.
Wadhamini wengine katika tukio hilo kubwa mwakani ni pamoja na Tigo (km 21) sambamba na wadhamini wenza ambao ni Simba Cement, Kilimanjaro Water, TotalEnergies, CRDB Bank na TPC Sugar Ltd.
Wasambazaji rasmi wa tukio hilo – GardaWorld Security, CMC Automobiles, Sal Salinero Hotel, Kibo Palace Hotel na Keys Hotel.
Mbio za mwaka ujao zinatarajiwa kufanyika Jumapili ya Februari 23, 2023 katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi ambapo washiriki watapata fursa ya kushiriki mbio ambazo njia zitakazotumika zimepimwa kwa mujibu wa kanuni za IAAF ambapo zitajumuisha washiriki wa mbio za kilomita 42 (Full Marathon), 21km (Tigo Half Marathon) na mbio za kilomita 5 (5km Fun run).
Mbio hizo huandaliwa na kampuni ya Kilimanjaro Marathon na kuratibiwa hapa nchini na kampuni ya Executive Solutions limited.