The House of Favourite Newspapers

Wabunge; hatutarajii zile ‘sinema’ zenu

0

TUMSHUKURU Mungu kwa kutuweka hai leo, hakika hana budi kuabudiwa milele duniani kote.

Baada ya kusema hayo nianze kwa kusema kwamba kuanzia leo Watanzania watakuwa wanafuatilia bunge letu linaloanza mjini Dodoma ambalo kwa kweli limekuwa tukufu kutokana na kuibua mambo mbalimbali yanayodidimiza nchi.

Wengi wetu bado tunakumbuka sakata la Escrow lilivyotikisa bungeni na wabunge wengi waliziacha itikadi zao na ‘kukomaa’ na ufisadi ule uliohusisha ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi za umma.

Pamoja na umahiri wa wabunge, bunge lililopita lilikuwa na vioja vingi na lilimlazimisha spika au naibu wake kutumia Kanuni za Bunge kuwatoa nje baadhi ikiwa kama adhabu.

Hatutarajii safari hii kuona vioja kama vile na badala yake tunategemea kuona wabunge wakishikamana kutetea mali za umma na kuisimamia vema serikali kama Katiba ya nchi inavyotamka.

Nawaomba wabunge wazingatie mambo matatu, kwanza watambue kuwa Bunge letu limewekewa mipaka mikubwa kikatiba katika kuiwajibisha serikali. Kikatiba, Bunge halina uwezo wa kumfukuza mtu yeyote kazi zaidi ya rais, waziri mkuu na spika.

 Bunge lina mamlaka ya kuwafukuza hawa kwa sababu bosi wa rais ni wananchi na Bunge linaweza kumfukuza kazi rais kwa niaba ya wananchi pia linaweza kumfukuza kazi waziri mkuu kwa sababu ndilo lilimthibitisha katika uteuzi wake. Kwa hiyo, kiufundi, waziri mkuu anateuliwa na mihimili miwili-Rais na Bunge.

 Bunge pia linaweza kumfukuza kazi spika kwa sababu ndilo lililomchagua. Kwa hiyo, tunapowakomalia wezi wa mali za umma wafukuzwe ni muhimu pia kuanza kufikiria namna ya kulipa meno zaidi Bunge katika Katiba Iliyopendekezwa.

Najua kuwa ‘kiporo’ cha Katiba Iliyopendekezwa ambayo imekwama kipo na inaweza kupitiwa upya.

Katiba hiyo kama haina mambo hayo, itakuwa sababu nyingine ya kuikataa. Niwaambie wabunge kuwa wakati umefika wa kuwekeza katika kuunda mfumo mzuri wa kuisimamia serikali.

 Niwaombe wabunge kwamba wasiwe wepesi wa kuhukumu, hoja ikija ichambuliwe bila kujali itikadi za kisiasa japokuwa najua kwamba raha ya majadiliano ni kwamba kuwe na hoja kinzani.

Kwa vyovyote vile tusiwachukulie viongozi wetu wa ngazi yoyote kama malaika ambao hawatafanya makosa, watafanya makosa na ni lazima tuwakosoe wanapokuwa wamekosea, lakini tuache tabia ya kutumia lugha za kuudhi na za kashfa.

Hakuna asiyejua kwamba wabunge wote mmefika ndani ya jengo hilo baada ya kuaminiwa na wananchi kwamba mtawasemea kero zao kwa viongozi wa serikali ili ufumbuzi upatikane. Itashangaza kuona mbunge anakwepa jukumu la kutetea wananchi eti kwa sababu hoja imetolewa na mbunge ambaye si wa chama chake.

Linapokuja jambo muhimu la kitaifa, itikadi ziwekwe pembeni na hapo ile kauli mbiu ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu itumike, kwa kufanya hivyo tutapiga hatua kusonga mbele kimaendeleo.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply