Wabunge, Madiwani Wahamiaji; Wana Kazi Kubwa Kupenya!

WABUNGE na madiwani wa vyama vya upinzani waliohamia CCM na wale waliohamia vyama vingine, wana mtihani mkubwa wakati huu tunapoelekea kwenye mchakato wa kupata watakaopeperusha bendera kugombea nafasi hizo.
Hatua ya madiwani na wabunge kuhama vyama vya upinzani na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni gumzo hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu baada ya kushuhudia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na CUF vikiwapoteza wabunge na madiwani baada na kabla ya bunge kuvunjwa.
Zaidi ya madiwani 146 wametajwa kuvihama vyama vya upinzani. Wabunge waliokuwa Chadema na CUF waliohamia CCM baadhi yao walipata bahati ya upendeleo kwa kuteuliwa na chama tawala kugombea bila kuwekwa kwenye kikapu cha kura za maoni, hivyo kupita kirahisi na kurudi bungeni.
Kwa mujibu wa vifungu vya 37 (1)b na 46(2) vya sheria ya uchaguzi, inaipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini kutangaza jimbo kuwa wazi na kuitisha uchaguzi mdogo mbunge anapotoka chama na tume ilifanya hivyo.
Hata hivyo, gumzo miongoni mwa wana CCM ni kuwa je, wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu 2020 wabunge na madiwani, watapenyezwa tena bila kupitia mchakato na wenyeji? Jibu ni kwamba, si rahisi kwani chama tawala kikifanya hivyo, kitajiangamiza na kuleta mpasuko.
Mjumbe mmoja wa Halmashauri Kuu ya Taifa, alimlalamikia Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli juu ya mtindo wa kupenyezwa ‘wanachama wageni’ kupata uongozi. Mwenyekiti alijibu kifupi kwamba, hilo limalizwe hukohuko mkoani.
Kwa vyovyote, wabunge na madiwani waliohamia CCM na hata waliohamia vyama vingine, itawabidi wapambane ili kuwashinda wanachama wenyeji ambao wana kiu ya kuwa wabunge au madiwani.
Waliohama wana mtihani mzito kwa sababu kuna kundi linaloamini kuwa wanasiasa hao walinunuliwa, jambo ambalo halijathibitishwa hadi leo kwa nyaraka zozote rasmi za manunuzi au kauli.
Kundi hili linaloamini kuwa wageni hawakuja kwa hiyari yao, lina mashabiki wengi kutoka chama tawala, wanaamini kwa kuwa hao wageni walipitishwa bila kuchujwa, kwenye mchujo watakuwa na kazi ya ziada kuwaaminisha wajumbe kwamba wanafaa kuendelea na ubunge au udiwani.
Lakini pia kuna wagombea wa upinzani wana wasiwasi kuhusu wasimamizi wa uchaguzi kwamba wanaweza kuwafanyia kitu mbaya.
Wanatolea mfano wa uchaguzi mdogo wa Korogwe-Vijijini ambapo mgombea wa Chadema aliambiwa amechelewa kuwasilisha fomu, hivyo mgombea wa CCM, Timothea Mzava kutangazwa kupita bila kupingwa kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Septemba 16, mwaka jana baada ya kujikuta pekee yake ametimiza sharti la kurudisha fomu muda wa mwisho Agosti 20, 2018.
Tukio hilo lililalamikiwa na Chadema wakidai mgombea wao, Amina Ally alifanyiwa hila. Hali hiyo imeibua mgawanyiko kwa sababu wananchi wapo makundi tofauti, hivyo kila upande unapata waungaji mkono na kuwa chanzo cha minyukano.
Kundi la tatu linaamini hamahama imetokana na vuguvugu la kisiasa linalotokea ndani ya vyama tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi. Kundi hili linatolea mfano uamuzi mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye ambao walihama CCM na kwenda Chadema miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na udiwani mwaka 2015 pamoja na wimbi la wanasiasa waliohamia upinzani mwaka huo.
Vilevile linajenga hoja kuwa katika utawala wa marais mbalimbali nchini Tanzania, kumekuwa na wimbi la wanachama wapya wanaopokelewa ndani ya CCM ingawa halikuwa jambo maarufu kama ilivyo awamu hii.
Kuna wananchi wengine wanasema hamahama hizo ndani ya vyama vya upinzani, inatokana na kuwa na migogoro ambayo huchochea baadhi ya wanasiasa kuhama.
Aidha, mgogoro wa Chama cha CUF, ulisababisha kumeguka makundi mawili, ya Katibu Mkuu Maalim Seif na Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba. CUF ya Maalim Seif lilikataa kumtambua Lipumba kwa kile kilichoeleza alijiuzulu mwenyewe mwaka 2015, hivyo hakuna kikao kilichoidhinisha yeye kurejea madarakani ndani ya chama hicho.
Mahakamani Lipumba alipewa chama, Maalim akahamia ACT-Wazalendo. Makundi hayo yanafanya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuwa mgumu hasa kwa wahamiaji waliotoka vyama vya upinzani kuhamia chama tawala.
‘Wahamiaji’ pekee ninaowaona wanapumua vizuri ni wa ACT-Wazalendo kwa sababu wabunge na madiwani wao wengi wamehama na wapiga kura wao.
Ni wazi kwamba wale waliohama peke yao na kuwaacha wapiga kura wao, itawabidi wafanye kazi ya ziada ili kujihakikishia ushindi maana walioachwa wanaona kama wameachwa solemba na wale waliowaamini awali. Bado kitambo kidogo tutashuhudia maajabu katika uchaguzi mkuu huu ujao.
Siasa za Siasa
Na Elvan Stambuli
Simu: 0655-339616

