The House of Favourite Newspapers

WABUNGE WALIONUSURIKA KIFO KATIKA AJALI

ROHO wa ajali ashindwe na pepo mchafu aenezae hofu kipindi cha mwisho wa mwaka ambapo ajali nyingi hutokea naye alegee; Mungu ajalie taifa letu kufunga mwaka salama.  Wakati tunaelekea kumaliza mwaka 2018 na kuingia 2019, bado ajali mbalimbali zimejeruhi ndugu zetu wengi na wengine kupoteza maisha. Kama taifa tunapoingia mwaka mpya ni vema tukakumbuka kuwa ajali ni adui wa ustawi wa taifa letu hivyo hatuna budi wote kuwa makini kuchukua tahadhari na kila liwezekanalo kuzuia zisitoke.

Wafuatao ni baadhi ya wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi walionusurika kufa kwa ajali; tumshukuru Mungu kwa ajili yao pamoja na wananchi wengine walionusurika kifo kwa ajali na tuwaombee wote waliopoteza maisha wapumzike kwa amani.

NAPE NNAUYE

September 24, 2018 Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Moses Nnauye alipata ajali ya gari katika Kijiji cha Kibutuka akiwa njiani kuelekea Liwale kwa ajili ya kushiriki kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Lindi. Mbunge huyo alinusurika kifo na kutoka salama. Hii ilikuwa ajali ya pili kwa Nape ambapo Oktoba 22, 2015, alinusurika kufa kwa ajali wakati akielekea jimboni Mtama Lindi akitokea jijini Dar es Salaam

HAMISI KIGWANGALLA

Agosti 4, 2018, Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini Dk. Hamisi Kigwangalla naye alinusurika kufa katika ajali mbaya ya barabarani katika Kijiji cha Magugu, Jimbo la Manyara baada ya gari la serikali alilokuwa akisafiria kupinduka.

JOSEPH MBILINYI ‘SUGU’

Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Januari 10,2015, alipata ajali ya gari katika eneo la Mlima Kitonga mkoani Iringa. Jambo la kumshukuru Mungu ni kwamba alitoka salama yeye na wenzake wanne waliokuwa kwenye gari alilopata nalo ajali.

ESTER MATIKO

Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, Februari 25, 2017 eneo la Kitambaa kilometa chache kutoka Mto Simiyu alipata ajali ambapo mtu mmoja alitajwa kupoteza maisha.

JESCA KISHOA

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Jesca Kishoa alilazwa katika Hospitali ya Bunge jijini Dodoma, Mei 11, 2018, baada ya kupata ajali eneo la Erea D akiwa njiani kwenda kuhudhuria kikao cha bunge.

PAULINA GEKUL

Mbunge wa Jimbo la Babati mjini, Paulina Gekul alinusurika kifo Februari 27, 2017, baada ya gari lake kupinduka mkoani Manyara.

Gari lake lenye namba za usajili T 189 BHQ liliacha njia na kupinduka ambapo mbunge huyo alikuwa katika msafara wa Naibu Waziri wa Mazingira (wakati huo) Luhaga Mpina.

JOSHUA NASSAR

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassar Julai 8, 2015, alinusurika kifo baada ya helkopta aliyokuwa akiitumia katika mikutano ya kuhamsisha zoezi la uandikishaji kupiga kura kuanguka muda mfupi baada ya kupigwa na kile kilichotajwa kuwa ni radi. Tukio hilo lilitokea katika eneo la Leguruki wakati helkopta hiyo iliyokuwa imebeba viongozi wa Chadema waliokuwa wameambatana na Nassar wakitoka katika mikutano hiyo.

  1. TULIA AKSON

NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson, alipata ajali Februari 24, 2016 mkoani Mbeya baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongana na gari jing dogo.

Dk. Akson alipata ajali hiyo eneo la Kipoke wakati akitoka mjini Mbeya kuelekea kijijini kwao Bulyaga, Wilaya ya Rungwe, alipokuwa akienda kwenye Shule ya Sekondari Loleza alikopata elimu yake ya sekondari miaka mingi iliyopita

SIKUDHANI CHIKAMBO

Toyota VX lenye namba za usajili T329 DGK alilokuwa akisafiria Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Ruvuma, Sikudhani Chikambo lilipata ajali Julai 7, 2017, eneo la Dumila, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro. Mbunge huyo pamoja na watu wengine watano walikuwa wakisafiri kutoka Dodoma kwenda jijini Dar es Salaam.

SULEIMAN JAFO

SEPTEMBA 6, 2016, Mbunge wa Jimbo la Kisarawe na Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo alinusurika kifo baada ya kupata ajali ya gari eneo la Katela Kata ya Kiwira, Wilaya ya Rungwe Mbeya. Ajali hiyo ilihusisha gari dogo aina ta Corolla iliyokuwa ikotokea Mbeya kwenda Rungwe.

CECILIA PARESO

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Cecilia Pareso na baadhi ya madiwani wa Karatu walinusurika katika ajali mbaya ya gari iliyotokea Desemba 31, 2016, eneo la Nanja wakati wakitokea Arusha. Katika gari hiyo, inaelezwa kuwa ilikuwa na jumla ya madiwani watano na mbunge Paresso wakitokea Arusha mjini kuwadhamini madiwani wenzao waliokuwa wamekamatwa na polisi.

Comments are closed.