The House of Favourite Newspapers

Wachagga Wanaporejea Nyumbani Krismasi, Mwaka Mpya!

mabasi

Na Walusanga Ndaki Gaztei la Risasi Jumamosi, Toleo la Desemba 24, 2016

ASUBUHI moja mwaka jana, wiki moja kabla ya Krismasi, Michael Ndashau, (51), analiingiza gari lake Toyota Land Cruiser kwenye lami nzuri ya Barabara ya Morogoro akitokea njia ya vumbi na makorongo ya King’ongo, Kimara, jijini Dar es Salaam.

Familia hiyo inaelekea kijijini Maili Sita, Kilimanjaro, kwa ajili ya Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Wakati taa za usiku zikiupamba Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Irene Mringo (48) mwajiriwa wa Umoja wa Mataifa jijini Abidjan, Ivory Coast, anateremka kwenye dege kubwa la Swissair na familia yake ya watu watano.  Wote wanatabasamu wakitegemea kukutana na ndugu zao waliokuja kuwapokea ili kesho yake waelekee nyumbani kwao Himo, kwa Krismasi na Mwaka Mpya!

mabasiiiMvua ya manyunyu inanyesha mpakani Namanga kati ya Kenya na Tanzania, ambako mzee Rodrick Sifuel na familia yake ya watu sita, wanachungulia nje ya madirisha ya gari  lao la Noah wakisubiri kukaguliwa.  Wanatokea Nairobi, Kenya, ambako mzee huyo ana maduka na sasa wanaelekea kijijini Machame kula Krismasi na Mwaka Mpya.

Makundi hayo ya “Wasafiri wa Desemba” (December Trekkers)  ni mfano halisi wa Wachagga walio nje ya nyumbani kwao (diaspora) waliozagaa Canada, Afrika Kusini, Uingereza, Marekani na kwengineko wakirejea nchi ya mababu zao “kuhesabiwa”.

Kwa miaka nenda-rudi utamaduni huo huwakusanya Wachagga  wasomi, wafanyabiashara na wa kawaida wakajikuta wakinywa Mbege na kutafuna Ndafu.

Mzee Barnabas Maro, mwandishi mkongwe nchini, aliwahi kuulizwa kuhusu marejeo hayo (Exodus)  ya Wachagga akayaunga mkono japokuwa yeye hafanyi hivyo.

“Huwa siendi Kilimanjaro kwani  sasa sina ndugu wa karibu aliyebakia huko,” alisema akiongeza kwamba sehemu kubwa ya maisha yake ameipitisha akiwa nje ya Kilimanjaro, hususan Dar es Salaam, hivyo hamu marejeo huko Moshi haiko sawa na Wachagga wenye ndugu huko.

“Hata nikienda Moshi ni watu wachache sana wanaonifahamu…” alisisitiza akiunga mkono utamaduni huo  ambapo Wachagga huutumia kutatua masuala ya kiutawala, kiutamaduni, kimila na kupata baraka kutoka kwa wahenga wao.

Joyce Temba, mfanyakazi wa Global Publishers Ltd, kampuni ya wachapishaji wa magazeti  yaliyotukuka ana mawazo yake kuhusu  safari hizo.

“Safari za Moshi nazipenda na naziunga mkono.  Nilikuwa nazifanya kila mwaka isipokuwa sasa ajira yangu inaniwia vigumu kwenda huko.  Lakini ni kitu ninachokipenda sana.

“Furaha ya kwenda huko ni kubwa. hunikutanisha na bibi na babu yangu kwa upande wa mama ambao wote bado wanaishi.  Hilo linanipa mimi na wao faraja kubwa, kwani kila familia hupata wageni wa aina hiyo wakati wa Krismasi na Mwaka Mpya,” anasema msichana huyo mwenye wajihi na umbo la kuvutia.

Anaongeza kwamba marejeo hayo Kilimanjaro huleta maelewano zaidi katika familia zilizokuwa na tofauti, pia fursa wanaorejea kuboresha au kukarabati makazi yao waliyoyaacha kwa mwaka mzima.

“Ni jambo lenye furaha kubwa kula na kunywa pamoja katika mkesha wa kuzaliwa kwa Yesu, na kuusubiri Mwaka Mpya,” anasema Joyce akiongeza kwamba anayeshindwa kwenda Moshi wakati huo atakuwa na sababu zake binafsi.

Naye Mhariri wa gazeti la Ijumaa Wikienda, Paul Sifael, anasema safari hizo ni utamaduni mwema wa kuwarejesha watu makwao kuonyesha walichokivuna ugenini baada ya kujituma.

“Ni tukio la mtu kwenda kuonyesha alichokipata baada ya kutumwa au kujituma kuondoka Kilimanjaro.  Ni muhimu pia kwani mbali na kuwakutanisha wahusika, linatoa pia fursa ya kutambulishana na kuwatambulisha watoto waliozaliwa ugenini.  Hili ni muhimu kuzuia watoto kuingia katika ndoa haramu kutokana na kutofahamiana,” anasisitiza Sifael.

“Ni historia nzuri inayoendeleza malezi kwa watoto wa Kichagga kujituma kwenda kusaka maendeleo na kurudi kuyaonyesha matokeo yake kwa ndugu zao katika sura  chanya ya kiuchumi,” anasema mhariri huyo.

Maureen Kirenga, nesi wa Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, mkazi wa Dar es Salaam ambaye hajaenda Kilimanjaro kwa miaka mingi ana mawazo yake.

“Wengi wao huenda kutanua tu, kuonyesha mapesa waliyovuna.  Mchagga lofa asiyeweza kununua hata mbege, haendagi Moshi wakati wa Krismasi, ” anasema kwa kicheko.

Mfanyakazi mwingine wa Global Publishers, Glory Massawe, anasifia ‘Exodus’ hiyo, japokuwa yeye hajafanya hivyo kwa miaka mingi.

“Unajua wazazi wote wa mama wamefariki, aliyebaki ni bibi yangu upande wa baba; naye yuko hapa Dar es Salaam.  Hivyo, utamu wa kwenda Moshi kwa kweli umepungua, kwani kilele cha furaha ni kushiriki na wazazi katika Krismasi na Mwaka Mpya,” anasema Glory akisisitiza tamaa ya kwenda Kilimanjaro kwake iko palepale akipata fursa.

“Ni jambo la kufurahisha pale waliopotea  wanaporudi na kuonyesha matokeo mema waliyoyapata katika kusaka maendeleo,” anasema.

Safari za kurejea Uchaggani mwisho wa mwaka zipo na zitaendelea kuwapo ambapo magari, ndege na usafiri mwingine huelekea eneo hilo lenye mlima mrefu zaidi Afrika – Kilimanjaro – na kulikutanisha kabila la watu wanaosemekana kuwa na mafanikio makubwa zaidi kiuchumi na kielimu nchini kuliko kabila lolote.

Marejeo ya Wachagga nyumbani kwao, yana utani kutoka kwa majirani zao Wapare wanaosema Wachagga wengi huzaliwa Septemba au Oktoba kwa vile wanaume wengi wa Kichagga hurejea kwa wake zao Desemba!

Kwa moyo wa kupenda nyumbani, Wachagga ni namba moja nchini. Makala hii inawatakia kila la heri wanaorejea Kilimanjaro kwa Krismasi na Mwaka mpya.

Kwa kina-Mangi na kina-Kadadaa, safari njema!

Haya ndo maisha halisi ya Ben Pol

Comments are closed.