Wachawi wamtaka Wastara akiwa bado tumboni
ILIPOISHIA…
MPENZI msomaji baada ya kuwa nami mwanzomwisho katika simulizi ya maisha ya Asha Baraka, mmiliki wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, nachukua wasaa mwingine kukukaribisha katika simulizi ya maisha ya muigizaji mwenye jina kubwa na heshima katika Tasnia ya Filamu Tanzania, Wastara Juma.
Wastara ni muigizaji aliyeanza kujipatia umaarufu zaidi akiwa chini ya kampuni ya kuandaa filamu iitwayo Wajey ambayo alikuwa akiimiliki pamoja na marehemu mumewe Juma Kilowoko ‘Sajuki’. Ameigiza muvi nyingi ikiwemo Mboni ya Jicho Langu, Vita, Detective na nyingine za hivi karibuni. Hapa anafunguka mwanzo mwisho historia ya maisha yake.
…SASA ENDELEA
“NIMEZALIWA mwaka 1983 huko Mvomelo mkoani Morogoro. Mimi ni mtoto wa tano kati ya saba wa mama yangu Hamida na baba yangu Juma Issa. Kabila la mama yangu ni Al Liwail na baba yangu ni Al Rawahi ambao asili yao ni huko Muscat, Oman.
“Hata hivyo nimechanganyikana na Wahindi na Wanyamwezi, kwa upande wa bibi aliyemzaa mama yangu, lakini bibi mzaa baba ni Mmasai. Wakati huo tunazaliwa, baba yangu alikuwa ni dereva na mama alikuwa akifanya biashara ya kuuza chakula,” anaanza kusimulia Wastara.
Wastara anaendelea kuwa katika maisha yake amepitia misukosuko mingi sana na yenye kuumiza. Anasema misukosuko hiyo ilianza hata kabla hajazaliwa maana aliwahi kusimuliwa na mama yake kuwa wakati akiwa na ujauzito wake wenye muda wa miezi sita, siku moja kuna sehemu alipita majira ya jioni.
Anasema sehemu hiyo ilikuwa ni ya vichaka na hakukuwa na watu wanapita mara kwa mara. Mama yake akiendelea kutembea Wastara anasimulia alihisi kuna watu walikuwa wanamfuata nyuma lakini alipokuwa akigeuka hakuwa anawaona.
“Sasa mama yangu ni mtu ambaye ni kama alikuwa na maono hivi. Japo alikuwa hawaoni watu hao lakini kwa namna mwili ulivyokuwa unamsisimka alifahamu wapo na walikuwa wakimfuatilia. Akaamua kuongea na kuwaambia wajitokeze ili wazungumze na kusema wanataka nini.
“Kweli baada ya kusema hivyo walijitokeza watu ambao anaamini walikuwa ni wachawi. Akawauliza wanataka nini w a k a m w a m bia wanamtaka mtoto ambaye alikuwa tumboni mwake maana alikuwa ni mzuri sana.
“Mama aliwakatalia na kuwaambia watahangaika sana lakini hawataweza kumpata mtoto wake. Baada ya kuwaambia hivyo wale wachawi walipotea na kumuacha akaondoka zake. Siku zikasonga mbele na hatimaye muda wa mama kujifungua ukawadia,” anasimulia Wastara.
Anaendelea kuwa siku chache baada ya kujifungua mama yake aliugua mno kiasi kwamba akawa hawezi kumnyonyesha kabisa kichanga wake. Wastara akawa analelewa na mfanyakazi wa ndani ‘housegirl’. Baada ya kuugua muda mrefu mama yake alipelekwa kwa mashehe na kufanyiwa dua ambapo baadaye akapona na kubeba ujauzito mwingine.
Lakini mtoto aliyejifungua alipatwa na matatizo makubwa ambayo alitakiwa kuyapata Wastara. Akiwa tu na miezi sita alianza kuugua ambapo hadi miaka miwili alikuwa hawezi kuzungumza na hali ikaendelea hivyo mpaka alipokuwa na miaka saba.
Wastara anaendelea kusimulia kuwa kwa upande wake ‘series’ ya misukosuko ilianza kutiririka, ukiachana na tukio la kutakiwa na wachawi akiwa bado mtoto mdogo sana ambaye hajafika hata umri wa kuanza shule.
Anasema wakati huo aliwahi kuugua ugonjwa wa Kifaduro ambao ulimsumbua mno. Anasema alikuwa kwenye hali mbaya kiasi kwamba alikuwa anajisaidia haja kubwa muda wote na popote pale. Wastara anafunguka wazazi wake walihangaika naye kwenye hospitali mbalimbali Morogoro lakini hakuweza kufanikiwa kupona. Akapelekwa Tumbi na hatimaye akapona alipofikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Siku zikaendelea kusonga mbele na baada ya kurudishwa nyumbani maisha yakaendelea. Sasa siku moja mimi na kaka yangu ambaye ninamfuata, tulikuwa tunaendesha matairi njiani. Ulikuwa ni mchezo wa kawaida tu ambao watoto enzi hizo walipendelea kufanya.
“Tukiendelea kuendesha mara kuna pikipiki ilikuja nyuma yetu. Tukawa tunakimbia kuikwepa lakini ikawa inatufuata tu. Tukienda upande wa kulia inatufuata, upande wa kushoto na bado inatufuata. Sasa mimi nikaamua kusimama katikati ya barabara. Ndipo ikaja na kunipitia PUUUU! Nikadondoka pembeni. Nilikuja kurejewa fahamu nikiwa katika Hospitali ya Bwagala iliyopo Turiani, Morogoro na nilikuwa nimevunjika miguu miwili.
“Hapo nilipewa tiba lakini sikuweza kufanikiwa kupona nikarudishwa nyumbani. Mwaka mzima ukakatika nikisota chini, nikawa mlemavu, kila kitu nikawa nasaidiwa hapohapo!”
Je, nini kitaendelea? Kipi kilitokea mpaka akapona tena miguu? Ni matukio gani ambayo mwanadada huyu amekutana nayo kwenye maisha yake? Usikose wiki ijayo.
Mwandishi: Boniphace Ngumije
Msimuliaji: Watara Juma
Makala Kutoka Gazeti la Championi Jumatatu | Staa anayefunguka