Makala: Gazeti la Championi, Toleo la Jumatatu, Januari 16, 2017
LONDON, England
DIEGO Costa kazingua tena. Kibaya zaidi katibua wakati Chelsea ikiwa imekoleza vita ya kuwania ubingwa wa Premier na yeye ndiye akiwa mchezaji anayetegemewa zaidi na klabu hiyo katika kupachika mabao.
Wiki iliyopita, straika huyo ambaye hadi juzi alikuwa kinara wa mabao kwenye Premier, alitoleana maneno makali na kocha wake Antonio Conte, kiasi cha kulazimika kutupwa nje katika kikosi kilichoivaa Leicester City juzi usiku.
Costa hakusafiri na kikosi cha Chelsea kilichokwenda jijini Leicester kuvaana na mabingwa hao watetezi kutokana na kutokukubaliana na mabosi wake kuhusu suala la majeraha yake.
Costa, 28, anaamini ana tatizo la mgongo wa chini ambalo linatokana na mfululizo wa matatizo ya nyama za paja ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.
Alitaka wiki iliyopita apumzike lakini Chelsea ilitarajia afanye mazoezi katika programu ya mazoezi magumu ya Conte, hata hivyo hakufanya mazoezi kwa siku tatu.
Kitendo hicho kilisababisha azozane kinoma na kocha wa viungo wa Chelsea na baadaye mzozo huo ukawa dhidi yake na Conte.
Tukio hilo limetokea siku chache baada ya Costa kupokea ofa nono kutoka China, huku ikiripotiwa kuwa kuna klabu moja imemwambia Mhispania huyo kwamba ipo tayari kumlipa kiasi cha pauni milioni 30 (karibu bilioni 80) kwa mwaka aondoke Stamford Bridge.
Hiyo itamaanisha kwamba atakuwa akipokea mshahara wa pauni 576,923 (Sh bilioni 1.5) kwa wiki, ambao hauko mbali na ule wa mwanasoka anayelipwa vizuri zaidi duniani, Carlos Tevez ambaye anapokea kitita cha pauni 615,000 (Sh bilioni 1.63) kwa wiki ambacho kinamfanya afanye chochote anachotaka kinachohitaji fedha katika dunia hii.
Inaaminika tayari wawakilishi wa Costa wapo China. Oscar na John Mikel Obi tayari walishaitosa Chelsea na kwenda kwenye dunia ya pesa (China).
Katika mzozo kati yake na Conte, kocha huyo Muitaliano ambaye naye ni mtata kwelikweli, inadaiwa alisikika akimbwatukia Costa akimwambia: “Nenda China tu.”
Klabu ya Tianjin Quanjian, ambayo imemsajili kiungo Mbelgiji, Axel Witsel, ipo sokoni ikisaka straika na imekuwa ikihusishwa na Costa kwa dau la pauni milioni 80.
Chelsea walikuwa na matumaini ya kukubaliana mkataba na Costa baada ya straika huyo awali kutamka kuwa ana furaha sana kuendelea kuichezea timu hiyo, lakini ishu hii iliyotokea wiki iliyopita imeibua utata.
C h e l s e a inatarajia suala hili liiishe haraka lakini limemuacha Conte akiwa na pasua kichwa kwa kuwa anataka timu yake irejee kwenye hali ya kushinda mfululizo.
Hadi kabla ya mechi za juzi, Costa alikuwa akiongoza kwa mabao kwenye Premier akiwa na mabao 14 na ilionekana kama nidhamu yake imepanda sana msimu huu, baada ya wakati fulani kucheza mechi 11 bila kuonyeshwa kadi, kitu ambacho kilikuwa nadra sana kwake katika misimu iliyopita.
Wawili hao walionekana kuwa na uhusiano mzuri, licha ya Costa kumbwatukia Conte katika ushindi dhidi ya Leicester mwaka jana, akionyesha ishara kwamba anataka kutolewa uwanjani ili kuepuka kupewa kadi na kuikosa mechi dhidi ya Manchester United kwa kuwa timu yake ilikuwa tayari na uhakika wa kushinda. Costa alionywa asirudie tabia hiyo.
Wiki moja tu iliyopita katika mchezo dhidi ya Tottenham ambao Chelsea iliambulia kipigo, Costa alikuwa katika sekeseke lingine baada ya kumbwatukia mchezaji mwenzake Pedro kwamba hakukimbia kwa mahesabu baada ya kupoteza nafasi. Conte alipuuza ishu hiyo akidai ni hali ya kawaida uwanjani.
Kuna matukio mengine mengi ya Costa kulianzisha mazoezini lakini yamekuwa yakitulizwa na kuzimwa kimyakimya.
Hata hivyo, inaonekana ni afadhali sana msimu huu kwa Costa ukilinganisha na msimu uliopita ambao alifikia hatua ya kumtupia nguo (bips) kocha wake Jose Mourinho kisa kumtoa nje, pia kugombana mazoezini na mchezaji mwenzake Oscar ambaye hivi sasa amekwenda China.
Suala la Costa linaweza kumshinikiza Conte atafute straika katika dirisha hili la Januari. Anavutiwa kumsajili Fernando Llorente kutoka Swansea na kumbakiza Michy Batshuayi ambaye anatakiwa kwa mkopo West Ham, Marseille, Paris St-Germain na Lille.
Lakini swali la wengi ni je, Chelsea itaweza kuendelea vyema katika mbio za ubingwa kama suala hili halitaisha haraka?