visa

Wachina Wanne Watimuliwa Kenya kwa Kumcharaza Mkenya

 

RAIA wanne wa China waliokamatwa na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wanatarajiwa kurudishwa kwao baada ya amri iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Fred Matiang’i.

 

 

Agizo hilo lilisainiwa na Matiang’i, juzi Jumatano, Feb. 12, 2020, baada ya mahakama kuruhusu polisi kuwashikilia Wachina wanne kwa siku 15 huku uchunguzi ukiendelea juu ya tukio la kumchapa viboko raia wa Kenya aliyekuwa akifanya kazi katika mgahawa unaoendeshwa na Wachina hao mjini Nairobi.

 

 

Wachina waliotambuliwa kwa majina ya Ou Qiang, Deng Hailan, Chang Yueping, na Yu-Ling; walitiwa nguvuni Jumapili baada ya video iliyoonyesha mmoja wa wahudumu wa mgahawa wa Wachina hao akipigwa viboko na mmoja wao  kuenea kwenye mitandao ya kijamii.

 

 

Katika video hiyo mwanaume wa Kichina alionekana akimpiga viboko Mkenya aliyekuwa akifanya kazi katika mgahawa unaouza vyakula vya Kichina, Chez Wou Restaurant, katika eneo la Kileleshwa jijini Nairobi.

 

Iliripotiwa kuwa Mkenya, Simon Oseko, alikuwa akichapwa viboko kwa kosa la kuchelewa kufika kazini. Alipigwa viboko viwili na meneja huku wafanyakazi wenzake wakishuhudia kwa mbali.

 

Oseko aliripoti tukio hilo katika kituo cha polisi. Iliripotiwa kuwa mpishi wa Kichina katika mgahawa huo pia aliwatisha wafanyakazi wengine raia wa Kenya ili wasizungumzie kuhusu mateso wanayopitia katika mgahawa huo.

 

Walikamatwa kwa kuwa na vibali vilivyokwisha muda waliopewa kuishi nchini Kenya na kufanya kazi nchini humo bila kuwa na vibali vya kazi.

 
Toa comment