Wachungaji Mashehe wakutana kanisani!
Na Dustan Shekidele, Morogoro
MIKAKATI! Katika kuhakikisha watumiaji wa madawa ya kulevya wanatoweka mijini, mapadre wa madhehebu mbalimbali wiki iliyopita walikutana na mashehe katika Ukumbi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Kihonda mkoani Morogoro ili kupanga mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo.
Habari zilizopatikana kutoka mjini hapa zinasema, viongozi hao wa dini walisema ni jambo la kusikitisha kwamba wao wanakwenda misikitini na makanisani kwa ajili ya kumtukuza Mungu, lakini wanashindwa kuwasaidia vijana wao wanaoangamia kwa matumizi ya madawa hayo ya kulevya.
Kwa mujibu wa kikao hicho, viongozi hao walikubaliana kufanya matamasha makubwa katika miji ya Morogoro na Dar es Salaam kwa lengo la kuwahamasisha vijana kuacha tabia ya kubwia unga.
“Itakuwa haina maana sisi viongozi wa dini tunakwenda makanisani na misikitini kusali wakati kundi la vijana wetu wanaangamia kwa kuvuta unga, moja ya majukumu ya viongozi wa dini ni kuwachunga waumini wake ambapo tunalazimika kuwafuata kondoo wetu waliopotea popote walipo na kuwarejesha kundini,” alisema mmoja wa viongozi hao, Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la KKKT Jimbo la Morogoro, George Pindua.
JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS